Mahakama mjini Paris- Ufaransa leo inataraji kutangaza hukumu dhidi ya mameya wawili wa zamani raia wa Rwanda wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya kimbari yaliyofanyika nchini Rwanda mwaka 1994.Upande wa mashitaka ulikuwa umeomba kifungo cha maisha dhidi ya mameya hao.
Kesi dhidi ya mameya hao wa zamani raia wa Rwanda imekuwa ikisikilizwa na mahakama ya mjini Paris-Ufaransa ;ambapo Bwana Octavier Ngenzi na Tito Barahira wanatuhumiwa kupanga na kuongoza mauaji dhidi ya watutsi katika wilaya ya Kabarondo mashariki mwa Rwanda.
Mameya hao waliongoza wilaya hiyo kwa kufwatana kwanzia mwaka 77 hadi 94.Kulingana na mwendesha mashitaka walitumia madaraka na uwezo waliokuwa nao na kuamuru mauaji makubwa yaliyotokea katika kanisa la Kabarondo tarehe 13 mwezi wa nne mwaka 94 .
Watutsi wapatao elfu mbili waliokuwa wamejificha ndani ya kanisa hilo waliuawa kwa siku moja.washitakiwa wanakana kuhusika kwao katika mauaji hayo.Kesi hii imedumu kwa miezi miwili ambapo pia walisikizwa mashahidi walioshuhudia mauaji ndani ya kanisa hilo.
Mwaka 2009 mameya hao wakiwa uhamishoni walihukumiwa na mahakama za jadi maarufu Gacaca kifungo cha maisha jela kwa kuwakuta na hatia ya mauaji ya kimbari .Hii ni kesi ya pili ya mauaji ya kimbari kusikilizwa na mahakama ya Ufaransa baada ya mahakama hiyo kutoa hukumu ya kifungo cha miaka 25 jela dhidi ya afisa wa zamani wa jeshi Captain Pascal Simbikangwa kwa hatia ya mauaji ya kimbari.
Post a Comment