0
KAMPUNI ya Vodacom Tanzania imezindua ofa mpya maalumu kwa wateja wake ambayo imetajwa kuwa inalenga kutimiza dhamira ya ubunifu wa teknolojia kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa gharama nafuu.
Huduma hiyo inayojulikana kama ‘Ya Kwako Tu’ ilizinduliwa juzi ikilenga kuwezesha wateja kujipatia vifurushi vya gharama nafuu kwa kadri ya matakwa yao kuanzia vya huduma ya data, kupiga simu na kutuma ujumbe mfupi wa maneno.
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom, Rosalynn Mworia, alisema kama mteja anapendelea vifurushi vya muda wa maongezi anapatiwa, badala ya kulazimika kuingizwa kwenye vifurushi vya data.
Atakayehitaji kununua vifurushi vya data hatalazimika kununua muda wa maongezi, kadhalika wanaohitaji vifurushi vya data na muda wa maongezi watapatiwa pia.
“Ofa hii imelenga kuleta unafuu kwa wateja wetu na kila mmoja atanufaika kwa kupata unafuu kadri ya matumizi yake na tunataka kuhakikisha kila mmoja anapata kifurushi kutokana na chaguo lake na huduma anayotaka na ndiyo maana ofa hii ni kwa ajili ya wateja wenyewe kama ilivyo jina lake la ‘Ya Kwako Tu’, yaani kwa ajili yako,” alisema Mworia.
Aliongeza kuwa, siku zote Vodacom inathamini wateja wake na muda wote imekuwa ikisikiliza matakwa yao ili wapate huduma bora kadri wapendavyo na ndiyo maana imewaletea ofa hiyo yenye kuleta unafuu, wakati huo huo kila mmoja akijipatia kifurushi kulingana na mahitaji yake.

Post a Comment

 
Top