Mamlaka ya mapato ya Rwanda imewataka wafanyabiashara wote hata wachuuzi wa rejareja kuanza kutumia mashine zinazotoa bili kielektroniki.
Huu ni mfumo ambao kawaida umekuwa ukitumiwa na wafanyabiashara wenye kipato cha wastani kwenda juu ambao pia hulipa kodi ya ongezeko la thamani (VAT).
Serikali inasema mfumo mpya utaiwezesha kuingiza pesa nyingi zitokanazo na ushuru ila baadhi ya wachuuzi wanasema mfumo huo utawaumiza.
Mashine zinazotoa bili kielektroniki hadi hivi sasa zimekuwa zikitumiwa na wafanyabiashara wapatao elfu 15 nchi nzima wenye kipato kikubwa na ambao tayari wamo katika mfumo wa kodi ya ongezeko la thamani ama VAT, lakini tayari agizo limetolewa kuwa lazima hata wachuuzi wa rejareja waingizwe katika mfumo huo wa kutoa bili kielektroniki.
''Tunataka kila mtu anayesfanya shughuli ya biashara kutumia mashine hii hata kama hayumo katika mfumo wa VAT .
Hii itatusaidia kukagua vizuri utoaji ushuru .Kujua hali halisi ya mapato ya kila mfanyabiashara.Hata kama utaingiza franga elfu 10 lakini kwa kutumia hii mashine ni vizuri sisi tujue kwamba umeingiza kiasi fulani au hujaingiza chochote''
alisema naibu kamishna mkuu wa mamlaka ya mapato ya Rwanda Pascal Ruganintwari.
Kutokana na upelelezi uliopo hapa dhidi ya wakwepa kodi baadhi ya wafanyabiashara wadogo wadogo niliozungumza nao wamejizuiya kubainisha kinagaubaga hisia zao.
Huyu amesema hawana budi kutimiza matakwa ya serikali: ''La muhimu ni kwamba siyo mimi pekee nitakayetumia mashine hii.kama ni mpango wa serikali lazima sote tuuheshimu.shida ni kwamba unaweza ukakuta kwamba mashinde yenyewe ni ghali kuliko hata biashara ninayofanya sasa kwa hiyo sijui kama kwanza nitauza bidhaa zangu zote ili kununua mashine ya kutoa bili au nitafanyaje,lakini ndiyo hivyo serikali ikiamua tunatekeleza tu''
''Hii itakuwa gumu kwetu na huu ni ukandamizaji kwa sababu siku nzima inaweza kumalizika bila kupata mteja hata mmoja.kuna wateja wengine wanaosema kwamba hawahitaji bili na pengine kunakuwepo na uelewano baina yetu na wateja.mimi nahisi hizi mashine zinazotoa bili kielektroniki zingeendelea kutumiwa na wafanyabiashara wakubwa wanaoingiza pesa nyingi lakini sisi rejareja ni kama kutuuwa kabisa'' alisema mfanyibiashara huyo ambaye hakutaka jina lake kutajwa.
Gharama ya mashine moja ni franga za Rwanda laki tatu ama dolla mia 400 za marekani ,lakini kwa wanaofanya biashara ya rejareja mamlaka ya mapato inasema watapewa mashine hizi kwa bure lengo likiwa ni kukusanya kiasi kikubwa cha pesa kwa taifa hili ambalo kwa mara ya kwanza bajeti yake itategemea asilimia 62 ya mapato ya ndani.
Uamuzi huu wa kutaka kila mfanyabiashara kutumia mashine zinazotoa bili kielektroniki umekuja wakati bunge la taifa likiwa limeidhinisha mswada wa sheria ya kupunguza adhabu kali iliyokuwa ikitolewa dhidi ya wafanyabiashara wanaokwepa
kutumia mashine hizi.wamekuwa wakitozwa faini iliyo kati ya milioni tano na ishirini franga za Rwanda ambazo ni kati ya dolla laki 6 na elfu 25 za Marekani.
Post a Comment