0
KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni imeweka msimamo wa kutohudhuria kikao chochote cha Bunge la Jamhuri ya Muungano kitakachoongozwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, kwa maelezo kuwa amekuwa akivunja demokrasia kwa kuwafanyia ubabe na kuwapendelea wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Msimamo huo ulitolewa jana na Kiongozi wa Kambi hiyo, Freeman Mbowe nje ya Ukumbi wa Msekwa ulio katika Viwanja vya Bunge, muda mfupi baada ya wabunge wanaoiunda kambi hiyo kutoka nje ya Bunge walipoona kuwa Naibu Spika ndiye aliyepaswa kuendesha kipindi cha maswali na majibu asubuhi.
Kwa mujibu wa Mbowe, hawataona tabu kuendelea na utaratibu huo wa kususia vikao vinavyoendeshwa na Dk Tulia hata kama itakuwa ni vipindi vyote hadi Bunge livunjwe kwa sababu lengo lao ni kupinga uonevu na ubabe anaowafanyia.
“Tunaenda nje ya maeneo haya ya Bunge kukutana na wabunge wenzetu waliofukuzwa ili tujadili mambo ya msingi ambayo ni pamoja na kuweka mkakati wa kuwazungukia wananchi kuwaeleza juu ya uonevu wa Naibu Spika wachukue hatua kwa sababu ndio waliotuchagua.
Tunaenda kumshtaki Dk Tulia kwa wananchi,” alisema. Alieleza kuwa, hawako tayari kuona Naibu Spika akiunga mkono kusimamishwa kwa wabunge muhimu wa kambi hiyo, hivyo kuendeleza mgomo huo hata kama utakuwa ukiwagharimu.
Alifafanua kuwa pindi atakapoongoza Bunge mtu mwingine watakuwa wakihudhuria kwa sababu wao hawajalisusia Bunge wala mtu mwingine isipokuwa Dk Tulia. Alisema makosa wanayodaiwa kuyafanya na kuadhibiwa yanafanywa na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi pia lakini wanashangaa wanaobanwa ni wao pekee.

Post a Comment

 
Top