WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameondoka nchini kwenda Lusaka, Zambia kuhudhuria mkutano wa 51 wa mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika ( AfDB). Majaliwa aliyeondoka jana kwa ajili ya mkutano huo unaofanyika leo nchini humo, anamwakilisha Rais John Magufuli.
Anafuatana na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji, wachumi kadhaa pamoja na wataalamu wa sekta ya fedha. Mkutano huo utakaofunguliwa na Rais wa Zambia, Edgar Lungu utajadili masuala ya nishati na mabadiliko ya tabia nchi.
Pia utahudhuriwa na marais Idriss Deby wa Chad, Paul Kagame wa Rwanda na Uhuru Kenyatta wa Kenya. Nigeria itawakilishwa na Makamu wa Rais, Yemi Osinbajo huku Msumbiji ikiwakilishwa na Waziri Mkuu, Carlos Agostinho do Rosário.
Watu maarufu waliothibitisha kuhudhuria mkutano huo ni pamoja na Kofi Annan, Ashish Thakkar, John Kufuor, Mary Robinson, Mo Ibrahim, Nancy Lee, Ngozi Okonjo- Iweala na Tony Elumelu.
Mkutano huo utakaofanyika kwenye kituo cha mikutano cha kimataifa cha Mulungushi , utahudhuriwa na washiriki zaidi ya 5,000 kutoka nchi 54 wanachama wa benki hiyo, washiriki kutoka nchi 26 ambazo si Afrika.
Washiriki wengine ni wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, wadau wa maendeleo na wawakilishi wa asasi za kiraia. Wengine ni mawaziri wa fedha, biashara na uchumi na wataalamu kutoka vyuo vikuu.
Post a Comment