UKANDA wa Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) umeanza kupata mafanikio baada ya wawekezaji kuanza kujenga viwanda vya kusindika mazao vitakavyoongeza ajira na soko la mazao ya wakulima hasa wadogo.
Viwanda vitatu vipya vya kusindika nyanya na mazao ya mifugo vimejengwa katika mkoa wa Iringa ulioko katika kongani ya Ihemi inayojumuisha mikoa ya Iringa na Njombe kupitia programu ya Sagcot, viwanda viwili na Morogoro uliopo katika kongani ya Kilombero, kiwanda kimoja.
Mkurugenzi Mtendaji wa Sagcot, Geoffrey Kirenga alisema hayo hivi karibuni mjini Njombe katika kikao cha mapitio ya utekelezaji wa programu ya Sagcot katika kongani ya Ihemi kilichohusisha wadau mbalimbali wakiwemo wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya za mikoa ya Iringa na Njombe.
Alisema Iringa Mjini kimejengwa kiwanda kipya chenye uwezo wa kusindika tani 200 za nyanya kwa siku na cha kusindika vyakula vya mifugo kwa kutumia mahindi, soya na mashudu ya alizeti chenye uwezo wa kuzalisha zaidi ya tani 130 kwa siku, wakati mkoani Morogoro kinajengwa kiwanda cha kusindika mazao ya mifugo hasa kuku na samaki.
Alisema kukamilika kwa viwanda hivyo mjini Iringa kumewaongezea soko wakulima wa Iringa, Njombe, Ruvuma na Mbeya wanaoweza kuvitumia kuuza zaidi ya tani 300 za mazao yao kwa siku.
Kirenga alisema katika mikoa hiyo yenye eneo linalozalisha asilimia 65 ya chakula kinachozalishwa nchini, mazao ya biashara na chakula kama mahindi, kahawa, mpunga na chai, sehemu yake kubwa yanauzwa yakiwa ghafi kwa sababu ya ukosefu wa viwanda.
“Kwa kuzingatia sera ya Rais John Magufuli, nchi hii imeanza safari ya uchumi wa viwanda ambayo sehemu kubwa itajengwa kutokana na kazi inayofanyika katika eneo hilo la kilimo la Sagcot kwa hiyo tunahitaji viwanda vingi zaidi vya kusindika mazao kuongeza thamani ya kile kinachozalishwa shambani,” alisema Kirenga.
Alisema programu ya Sagcot inayohusisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Iringa, Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Njombe na Katavi iliyogawanywa katika kongani sita za Ihemi, Rufiji, Kilombero, Mbarali, Ludewa na Sumbawanga, ilianza kutekelezwa mwaka 2011.
Post a Comment