Arsenal wanakaribia kufikia makubaliano ya kumnunua mshambuliaji matata kutoka Gabon Pierre-Emerick Aubameyang kutoka Borussia Dortmund kwa karibu £60m.
Lakini uhamisho huo hautaidhinishwa hadi pale Dortmund watakapopata mchezaji wa kujaza pengo ambalo litaachwa na Aubameyang.
Taarifa zinasema mshambuliaji wa Arsenal Olivier Giroud ni miongoni mwa wachezajia ambao wanatafutwa na klabu hiyo ya Ujerumani.
Gunners tayari walikuwa wamewasilisha maombi ya kutaka kumchukua Aubameyang mara mbili lakini yakakataliwa na Dortmund.
Aubameyang, 28, alianza kwenye mechi Dortmund kwa mara ya kwanza tangu 16 Desemba mnamo Jumamosi katika mechi ambayo walitoka sare na Freiburg.
Dortmund wamesema wako tayari kumuuza mchezaji huyo lakini iwapo "matakwa fulani yatatimizwa kikamilifu".
Klabu hiyo ya Bundesliga ilikataa ofa ya euro 50m (£43.64m) kutoka kwa Arsenal Jumatano.
Aubameyang alikuwa anatumikia anatumikia adhabu na hakuruhusiwa kucheza mechi yao dhidi ya Wolfsburg wiki mbili zilizopita baada yake kukosa kuhudhuria mkutano wa timu hiyo.
- Wenger athibitisha Arsenal wanamtafuta Aubameyang
- Dortmund: Hakuna mazungumzo ya kumuuza Aubameyang
- Arsene Wenger adaiwa 'kuikosea heshima' Dortmund
Mshambuliaji huyo wa Gabon pia aliachwa nje ya kikosi cha klabu hiyo kilichocheza dhidi ya Hertha Berlin wikendi iliyopita kwa sababu maafisa wa klabu walihisi kwamba hakuwa ameangazia mechi hiyo kikamilifu, lakini alicheza dakika 90 katika mechi hiyo dhidi ya Freiburg.
"Tuko tayari kukamilisha uhamisho lakini ikiwa matakwa fulani yatatimizwa kikamilifu," mkurugenzi wa michezo Michael Zorc aliambia runinga ya German TV.
"Tuna msimamo ulio wazi. Arsenal wamefanya majaribio kadha kufikia sasa. Lakini tumeyakataa yote."
Arsenal wanamtafuta Aubameyang kujaza nafasi iliyoachwa na mchezaji wa Chile Alexis Sanchez aliyejiunga na Manchester United mapema mwezi huu kwa kubadilisha na kiungo wa kati Henrikh Mkhitaryan.
Aubameyang, 28, ni stadi sana kwa kufunga mabao na mwandishi wa BBC Stanley Kwenda anasema bila shaka anaweza kufaa klabu hiyo ya England ambayo msimu huu imetatizika kufunga mabao.
Kufikia sasa msimu huu Aubameyang amefunga mabao 13 katika mechi 15 alizocheza.
Alifunga mabao 31 katika mechi 32 msimu uliopita na kwa sasa amepungukiwa na mabao mawili pekee kufikisha mabao 100 aliyoyafunga tangu atue Ujerumani mwaka 2013.
Duru Ujerumani zilikuwa awali zinasema itawagharimu Arsenal zaidi ya £50m kumtoa mchezaji huyo Borussia Dortmund wakifanikiwa.
Post a Comment