0
KLABU ya Yanga ipo kwenye hati hati ya kuburuzwa kwenye Mahakama ya Kibiashara na wadhamini wao Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kwa kuvunja mkataba.
Habari za uhakika kutoka ndani ya TBL zimeiambia HabariLeo kuwa, kampuni hiyo inakusudia kuiburuza Yanga mahakamani kutokana na kushindwa kutimiza matakwa ya mkataba wake.
“Hatua ya makundi ambayo Yanga wamefika ilikuwa ni muhimu sana kwa mdhamini wao kumtangaza, lakini badala yake wameingia hatua hiyo wameondoa nembo ya mdhamini wao, wakati bado wapo ndani ya mkataba. “TBL inakusudia kuiburuza Yanga Mahakama ya Biashara, mwezi mmoja uliobaki ulikuwa na manufaa zaidi kwa wadhamini na maana kubwa kuliko kipindi chote ambacho wamewadhamini,”alisema ofisa huyo.
“Cha kushangaza wameenda Algeria wameondoa nembo ya mdhamini kifuani, na siku za hivi karibuni wamekuwa na maelewano ambayo sio mazuri na wadhamini, ”alisema.
Yanga pamoja na kwamba haijatangaza rasmi kuvunja mkataba na TBL, tayari wameanza kuutumikia mkataba wa Quality Group Limited inayomilikiwa na mwenyekiti wake Yusuf Manji.
Tayari Yanga imeanza kutumia jezi zenye nembo ya Quality Group katika mchezo wao wa kwanza hatua ya makundi katika michuano ya Kombe la Shirikisho walipomenyana na Mo Bejaia ya Algeria na kunyukwa bao 1-0.
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji kupitia taarifa yake ya hivi karibuni alisema, “Mkataba wa Yanga na TBL uliosainiwa miaka mitano iliyopita na mtangulizi wangu ulikuwa ni haramu, kwani mamlaka ya kutia saini kwa mujibu wa katiba ya Yanga yapo kwa bodi ya wadhamini. “Nimejitahidi kurekebisha tofauti zote zilizokuwepo, lakini nimeshindwa, TBL ni mara moja tu imetoa Sh milioni 20 za Yanga Day, zilizoahidiwa kutolewa kila mwaka, haijalipa fedha ya marekebisho inayofikia Sh milioni 30 wala haijatupa basi kwa kiwango sahihi tulichotaka kama aliloahidi katika mkataba.
“Tumeijulisha TBL kuhusu hilo mara kwa mara, lakini hatujajibiwa, Yanga imeingia mkataba na kampuni ya masoko Internationala Marketing ili kupunguza pengo la udhamini wa TBL kwa ajili ya mishahara ya mwezi Juni, na ufadhili huu ni wa mwezi mmoja, jambo ambalo lilifanya Yanga kuvaa jezi za nembo yake katika mchezo dhidi ya TP Mazembe,”ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya Manji.
Hata hivyo, mkataba wa Yanga na TBL haujamalizika kama inavyosemekana na kwamba unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi huu, Julai 31. Tayari, klabu hiyo ya Jangwani wameondoa nembo ya Kilimanjaro kwenye basi aina ya Yutong waliyopewa na TBL kama sehemu ya udhamini wao kwa klabu hiyo ya Jangwani, ambayo waliidhamini kwa jumla ya Sh bilioni 5 kwa miaka mitano.
Hivi karibuni Yanga ilikuwa ikishinikiza TBL irekebishe mkataba wake na kuwaongezea kiasi cha fedha.
Mkataba TBL ulikuwa ikigharamia mikutano ya mwaka ya klabu hizo mbili zenye wapenzi wengi hapa nchini na pia klabu hizo zitapatiwa kila moja Sh milioni 20 kwa ajili ya shughuli ya kuandaa matamasha ya klabu hizo, ambapo Simba wataandaa tamasha linalojulikana kama‘Simba Day’ ambalo litafanyika Agosti 8 kila mwaka, ingawa Yanga haijawahi kufanya matamasha.
Pia TBL imekuwa ikitoa vifaa vya michezo vyenye thamani ya Sh milioni 35, ambavyo vitatolewa mara mbili kwa mwaka kwa ajili ya kutumiwa na timu hizo kwenye michuano ya ligi na ile ya kimataifa. Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alisema kuwa yeye hajui lolote kuhusu mkataba huo na kwa sasa yuko safarini na aulizwe katibu.
Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit alisema mkataba wao umemalizika, hivyo hawana haja ya kuendelea kuutangaza lakini sasa wanamdhamini mpya na wakikamilisha watamtangaza.

Post a Comment

 
Top