KAMPUNI ya simu za mikononi ya Vodacom imetoa Sh milioni 6 kudhamini safari ya mafunzo ya waandishi 24 wa habari za michezo Nairobi, Kenya.
Waandishi hao kupitia Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (Taswa), ambao wamepata mwaliko kutoka kwa chama cha Kenya (SJAK), watakwenda jijini Nairobi kwa ziara hiyo ya mafunzo.
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom, Jacqueline Materu alisema, “Tumeona hii ni fursa njema kusaidia ziara hiyo ambayo itakuwa na faida katika maendeleo ya tasnia ya habari pamoja na michezo.”
Kwa upande wa Taswa, Makamu Mwenyekiti, Egbert Mkoko aliwashukuru Vodacom kwa udhamini huo ambao alisema wameonesha undugu wa damu.
Alisema waandishi hao wa michezo watatumia fursa hiyo kujifunza masuala mbali mbali ikiwemo kudumisha mahusiano na wenzao wa Kenya na pia mbali na mafunzo kutakuwa na michezo mbali mbali ya kirafiki ikiwemo soka. Kikosi hicho cha waandishi wa habari kitaondoka nchini Julai 8 hadi 10.
Post a Comment