0
MGONJWA mwenye maambukizi ya virusi vya Ukimwi ambaye pia ana homa ya uti wa mgongo, anashauriwa kutibu kwanza homa hiyo kabla ya kutumia dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi (ARVs) ili waweze kuishi muda mrefu, imeelezwa.
Daktari kutoka Taasisi ya Afya Ifakara, Andrew Katende alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu Ukimwi na uti wa mgongo, katika mkutano ulioandaliwa na taasisi hiyo kwa lengo la kuongeza ufahamu katika eneo la afya.
Alisema mgonjwa mwenye homa ya uti wa mgongo, anapoanza kutumia dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi, bila kuutibu uti wa mgongo yupo kwenye hatari ya kifo kwa asilimia 50.
Alishauri madaktari wanapomgundua mgonjwa aliyeathirika na Ukimwi kabla ya kumpa ARVs, wanapogundua ana fangasi inabidi wampime uti wa mgongo na kumpa tiba mapema ili aweze kuendelea na dozi hiyo nyingine.
Aliongeza kuwa kutibu ugonjwa huo wa uti wa mgongo ni shida hivyo inabidi kila mmoja achukue tahadhari asiupate kwa kuepuka kuvuta hewa yenye fangasi inayotokana na kinyesi cha njiwa.
Dk Katende alisema kutokana na utafiti walioufanya mwaka 2000, mkoa wa Dar es Salaam uliongoza kwa maambukizi ya ugonjwa wa uti wa mgongo pamoja na Ukimwi kwa asilimia 90, Ifakara ilikuwa asilimia 39 na kwamba takriban watu milioni moja duniani wanapata ugonjwa wa uti wa mgongo unaosababishwa na fangasi, kati ya hao wanaokufa ni 500,000.
Alisisitiza kuwa ni muhimu kupima ugonjwa huo wa uti wa mgongo mapema kwani kila anayeupata kama asipogundulika haraka hufariki. Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Honorati Masanja alisema wapo katika mkutano huo kwa ajili ya kubadilishana mawazo na kupeana uzoefu kwa mambo wanayoyafanya kila siku.
Alisema wana taasisi tano ambazo zipo sehemu moja zinazotoa huduma za afya, mafunzo na utafiti ndio maana wanaona wameona umuhimu wa kufanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya kuboresha maisha ya watu wa Bonde la Ifakara.

Post a Comment

 
Top