0
Rais John Magufuli amemteua Jaji Paul Kihwelo kuwa Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Ferdinand Wambali aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Taarifa kutoka Ofisi ya Jaji Mkuu Dar es Salaam kwa vyombo vya habari, ilisema kabla ya uteuzi huo Jaji Kihwelo alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania mkoani Iringa.
Kwa mujibu wa taarifa, Jaji Kihwelo pia aliwahi kuwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria kati ya mwaka 2009 na 2010, katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na aliwahi pia kushika nafasi ya Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Kudhibiti Viwango na Ubora.
Taarifa hiyo ilisema Jaji Kihwelo alipata Shahada ya Uzamivu ya Sheria (PhD) katika Chuo Kikuu Huria mwaka 2009, Shahada ya Uzamili ya Sheria (LL.M) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 2000 na Shahada ya kwanza ya Sheria (LL.B) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1997.
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kilianzishwa mwaka 1998 na kilianza kutoa mafunzo mwaka 2000.


Chuo kinatoa mafunzo ya Stashahada ya Sheria na Cheti au Astashahada ya Sheria, ambapo kina jumla ya wanafunzi 514 wanaoendelea na masomo kwa ngazi hizo. Kadhalika chuo kinatoa mafunzo endelevu kazini kwa majaji, mahakimu na maofisa wa mahakama.

Post a Comment

 
Top