0
TAASISI ya Sayansi za Bahari (IMS) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, imepeleka sampuli ya mwani nchini Norway ili kubaini aina ya mwani huo na sumu yake inayosababisha wakulima wa zao hilo kupata ukurutu.
Hayo yamebainishwa na Mhadhiri Mwandamizi wa IMS, Dk Avit Mmochi wakati akizungumzia athari za mwani pori kwenye Maonesho ya 40 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere Dar es Salaam.
Akizungumzia athari za kilimo cha mwani nchini katika mikoa ya Pwani na Zanzibar, Dk Mmochi alisema zao hilo limekumbwa na uvamizi wa mwani pori ambao unaua mwani halisi na kuleta madhara kwa wakulima wa zao hilo ambao hupata ukurutu wanapougusa mwani pori katika maji.
Alisema uvamizi huo ulianza kuibuka kidogokidogo miaka miwili iliyopita, lakini sasa athari yake inaendelea kuongezeka na kuleta madhara kwa wakulima pamoja na kupunguza uzalishaji wa zao hilo muhimu kwa uchumi wa nchi na wananchi.
“Tuna changamoto ya kuvamiwa na mwani pori, tumefanya utafiti wa awali tumebaini ni mwani pori jamii ya Lingbia ila tumemtuma mwanafunzi wetu Norway ambaye ameenda na sampuli ya mwani huo kufanya utafiti kwenye maabara, kubaini aina kamili ya mwani huo na aina ya sumu iliyoko ,inayosababisha wakulima kupata ukurutu,” alisema.
Alisema mwani unalimwa zaidi kwenye maeneo ya Pwani eneo la Songosongo, Kilwa na vijiji vya Jambiani, Paje na Bweleo Zanzibar.
Hata hivyo, alisema utafiti wa awali unaonesha kuwa uvamizi huo unatokana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na uchafuzi wa mazingira. Zao la mwani ambalo hutumika kutengeneza dawa na vipodozi ni la pili kwa kuingiza fedha za kigeni visiwani Zanzibar na la tatu baada ya utalii na karafuu.

Post a Comment

 
Top