0

MASTRAIKA kadhaa wapya wa kigeni kutoka nchi mbalimbali, wanatarajiwa kutua Ijumaa Dar es Salaam kufanya majaribio katika timu ya Azam FC.
Akihojiwa na radio moja nchini, Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba alisema mastraika hao watatua kufanya majaribio chini ya makocha wa Hispania na ikiwa watafuzu watasajiliwa.
Kawemba alisema kuna uhitaji mkubwa wa mastraika na kipa ambapo wanaendelea na mchakato wa kuwatafuta walio bora kuongeza nguvu katika kikosi hicho ili kufanya vyema msimu ujao.
“Tayari kuna wachezaji wawili wa kigeni ni makipa mmoja kutoka Hispania Juan Gonzalez na kutoka Ivory Coast Daniel Yeboah,”alisema na kuongeza kuwa nafasi inayohitajika ni ya kipa mmoja atakayesaidiana na Aishi Manula.
Mtendaji huyo alisema uhitaji wao upo katika nafasi za ushambuliaji ambapo ikiwa wachezaji wapya wataonesha kiwango kitakachohitajiwa na makocha hao basi watachukuliwa.
Pia, alisema katika nafasi ya kiungo wapo wengi huku akiweka wazi kuwa hawajitaji kuongeza na kwamba mchezaji wao Frank Domayo bado ana mkataba endelevu hivyo atakuwepo msimu ujao.
Alisema wachezaji waliopewa barua hadi sasa ni Said Morad na Didier Kavumbagu na wengine watapewa baadaye, baada ya kutazamwa na Kocha Mkuu Zeben Hernandez na Msaidizi wake Yeray Romero.
Kikosi cha Azam kilikuwa kianze mazoezi rasmi jana lakini kutokana na sikukuu ya Idd el Fitri wataanza leo kwenye uwanja wao wa Azam Complex, Chamazi.

Post a Comment

 
Top