SERIKALI imehimiza wadau, makampuni kuona umuhimu wa kudhamini timu za michezo mbalimbali ziweze kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari juzi wakati anaiaga timu ya vijana ya wanawake Vito Fc, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura alisema kuna umuhimu wa kusaidia timu za michezo tofauti badala ya kutegemea serikali peke yake kubeba mzigo huo.
Wambura aliulizwa, nafasi ya serikali kuisaidia timu ya ngumi za kulipwa kushiriki mashindano ya kufuzu Olimpiki, ambapo alisema wadau wanahitaji kuunga mkono na kuzisaidia timu.
“Nchi haijengwi na serikali peke yake, bali watanzania wote hivyo, wadau tunawahimiza kutambua umuhimu wa michezo mingine katika kulisaidia taifa na kuwezesha kusonga mbele,”alisema.
Kauli ya Wambura imekuja ikiwa ni siku chache, Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT) kutangaza kuwa limeshindwa kupeleka mabondia wawili wa ngumi za kulipwa katika mashindano ya kufuzu Olimpiki yanayofanyika Venezuela.
Mabondia waliotakiwa kwenda kushiriki mashindano hayo ni Thomas Mashali na Amos Mwamakula lakini ukata wa fedha uliwakwamisha.
Hata hivyo, Waziri huyo alisema watafanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga kuangalia lile linalowezekana. Mpaka sasa hakuna bondia yeyote wa ridhaa au kulipwa Tanzania aliyefuzu mashindano ya Olimpiki hivyo, hakutakuwa na mwakilishi wa mchezo huo mwaka huu.
Post a Comment