0
MSHAMBULIAJI wa zamani wa klabu ya Simba, Adam Kingwande amemwaga wino wa kuichezea Stand United kwa mwaka mmoja akitokea Kagera Sugar.
Stand inayodhaminiwa na kampuni ya uchimbaji wa madini ya ACACIA imeanza kujipanga kwa ajili ya msimu ujao baada ya kuwasainisha wachezaji waliofanya vizuri katika ligi iliyomalizika.
Mbali na Kingwande wachezaji wengine waliosajiliwa ni Erick Mlilo na Miraji Maka toka Toto African ya Mwanza.
Ofisa Habari wa klabu hiyo, Deo Kaji aliiambia HabariLeo, kuwa usajili huo umezingatia matakwa ya kocha wao Mfaransa Patrick Liewig kwa kuziba sehemu zenye mapungufu ndani ya kikosi hicho.
“Ripoti ya mwalimu ndiyo tunaifanyia kazi, tunaendelea kujipanga kwa ajili ya msimu ujao na bado tunawaangalia wachezaji wengine wa kuwaongeza,” alisema Kaji.
Alisema mbali na wachezaji hao pia timu hiyo ya wapigadebe wa Shinyanga maarufu ‘Chama la Wana’ wapo katika hatua za mwisho za kuingia mkataba na kocha msaidizi raia wa Ufaransa Guillaume Denis ambaye atakuwa pamoja na Athumani Bilali kumsaidia Liewig.
“Mazungumzo yanaendelea vizuri muda si mrefu tutaingia naye mkataba kwa ajili ya kuitumikia timu yetu msimu ujao, lengo letu ni kuhakikisha tunaleta upinzani na kufanya vizuri msimu ujao wa ligi.” alisema

Post a Comment

 
Top