0
WABUNGE na Wawakilishi wamepongezwa kwa kuishawishi jamii kujenga mazingira ya kuijua zaidi elimu ya dini ya kiislamu kupitia mashindano ya kisomo ya Kurani yaliyohusisha vijana wa vyuo vya elimu ya dini ya Kiislamu maarufu kama Madrasa, visiwani hapa.
Hayo yalisemwa na Katibu wa Mufti Mkuu, Shehe Fadhil Soraga, wakati akitoa hotuba katika ibada ya sala ya Idd el Fitr katika viwanja vya Mnazi Mmoja, mjini hapa.
Alisema mfano uliooneshwa na viongozi hao ndiyo wosia ulioachwa na kiongozi mkuu wa dini ya Kiislamu duniani, Mtume Muhammad (S.A.W) na maswahaba wake kukihifadhi kitabu hicho ili kiwe muongofu kwa watu wengine.
Alisema mashindano ya Kurani katika vyuo mbalimbali yanawaweka wanafunzi hao katika mazingira mazuri ya kufanya vizuri pia katika shule za msingi na sekondari.
“Tunawapongeza kwa dhati kubwa viongozi wetu ikiwemo wabunge na wawakilishi kwa kufanya kazi kubwa ya kuishawishi jamii katika mashindano ya kisomo cha Kurani. Hatua hiyo, imewawekea mazingira mazuri wanafunzi hao kufanya vizuri pia katika masomo yao,” alisema.
Aidha, Shehe Soraga aliwataka Waislamu kujiepusha na matendo ya kishetani ambayo kipindi chote cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani waliyaacha kutokana na utukufu wa mwezi huo.
“Ibilisi sasa yupo huru tayari kupotosha wananchi kwa sababu Mwezi Mtukufu wa Ramadhani umemalizika. Msikubali kurudi katika maovu, kwani anayemuasi Mungu katika kipindi cha Idd ni sawa na aliyemuasi siku ya kiama,” alisema shehe huyo.
Alikemea matukio ya hujuma zinazotokea Pemba zikiwamo za watu kukata mikarafuu ya wenzao kwa sababu za kisiasa na chuki. “Nayasema haya kwa uchungu mkubwa, matukio hayo Mungu haridhiki nayo tuache mara moja,” alisema shehe.

Post a Comment

 
Top