0
SHIRIKA la Maendeleo ya Taifa (NDC), limekifufua kiwanda cha kutengeneza vipuri na mashine cha Kilimanjaro Machine Tools Limited (KMTC), kwa kuanza uzalishaji wa mashine mbalimbali.
Akizungumza kwenye viwanja vya Maonesho ya 40 ya Biashara ya Kimataifa jijini Dar es Salaam, Meneja Mawasiliano wa NDC, Abel Ngapemba, alisema kiwanda hicho kimeanza uzalishaji wa mashine mbalimbali kama vile za kuranda mbao, kusaga na nyingine, ikiwa ni hatua ya kuachana na uagizaji wa mashine hizo nje.
Alisema mkakati wa sasa wa NDC ni kufunga mashine ya kuyeyushia vyuma ambayo thamani yake ni Sh mil 450, itakayotumika kutengenezea vipuri vya chuma vyenye maumbo tofauti kulingana na mahitaji ya mashine husika.
“Tumefanikiwa kufufua kiwanda cha KMTC Moshi na sasa uzalishaji wa mashine mbalimbali umeanza. Pia tuko mbioni kufunga mashine ya kuyeyushia vyuma ili tuweze kutengeneza vupuri mbalimbali na tuache kuagiza kutoka nje”, alisema Ngapemba.
Alisema juhudi zinaendelea za kuhakikisha kiwanda hicho kinakuwa moja ya viwanda vikubwa vya kutengeneza vipuri na mashine mbalimbali nchini, ambapo wamepata mbia kutoka moja ya mifuko ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya kuwekeza zaidi kwenye kiwanda hicho.
Alisema ifikapo mwakani, kiwanda hicho kitakuwa kimeanza rasmi uzalishaji wa vipuri vyote vya mashine tofauti nchini, hivyo kusitisha uagizaji wa vipuri kutoka nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, Ngapemba alisema kiwanda hicho kitaanza utengenezaji wa rimu za magari baada ya kiwanda cha matairi cha General Tyre kufufuliwa, hatua ambayo itaongeza soko la rimu na matairi nchini, hivyo kuachana pia na uagizaji nje.
“Kiwanda cha matairi cha General kitaanza kazi baada ya kukamilisha mambo ambayo hayajawa sawa, na nia yetu kiwanda hicho kikianza uzalishaji wa matairi na hiki cha KMTC, nacho kianze uzalishaji wa rimu za magari, tuachane na uagizaji wa nje,” alisema Ngapemba.
Alisema hilo linawezekana kwa kuwa Tanzania ina rasilimali ghafi nyingi kama vile chuma cha Liganga na kwamba mradi huo wa chuma nao uko mbioni kuanza na hivyo miradi yote hiyo ikianza kutekelezwa nchi itakua katika sekta ya viwanda na hivyo kufanya uchumi kukua Zaidi.
“Hapa ndio tutaona mapinduzi ya viwanda ambayo Rais John Magufuli anazungumzia kuwa nchi ya uchumi wa kati wa viwanda, na hili linawezekana kwa kufufua viwanda vyetu, na sisi NDC, tumeanza kutekeleza,” alisema Ngapemba.
Alisema mashine zinazotengenezwa katika kiwanda cha KMTC zina soko ndani ya nchi na kwamba wateja wengi wanazinunua kwa kuwa zina ubora na gharama nafuu kuliko kuagiza nje ya nchi.

Post a Comment

 
Top