0
Halmashauri ya wilaya ya Mkalama mkoani Singida, imerudisha zaidi ya shilingi 12.1 milioni TASAF makao makuu ambazo hazikupokelewa na walengwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya imani potofu kuwa fedha hizo ni za ‘freemason’.
Hayo yamesemwa juzi na mratibu wa TASAF wilaya ya Mkalama, Athman Dulle,wakati akitoa taarifa yake fupi ya utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini muda mfupi kabla ya kufunguliwa kwa mafunzo ya wataalam 24 wa ugani wa halmashauri hiyo.
Alitaja sababu zingine zilizochangia fedha hizo zisipokelewe na walengwakuwa ni vifo,kuhama kwa kaya na baadhi ya walengwa kutopata taarifa ya siku za kulipa/kutoa ruzuku hizo.
Dulle alisema pamoja na changamoto hiyo, halmashauri hiyo kuanzia Septemba 2014 hadi sasa, imefanya malipo mara 11 na jumla ya shilingi 2,136,625,570 zimelipwa kwa walengwa waliopo kwenye vijiji 42, ambayo ni sawa na asilimia 99.4 ya lengo.
Dulle alisema pia kupitia mpango wa TASAF 111, wanaendelea kujenga zahanati katika kijiji cha Kidarafa ambayo ujenzi wake utagharimu zaidi ya shilingi 71.6 milioni, jengo hilo kwa sasa lipo hatua ya kupuwa.
Kuhusu mafanikio mengine, mratibu huyo alisema kaya nyingi kwa sasa zimemudu kulima mazao ya chakula na biashara na hivyo zimejiongezea kipato, na zinamudu kupata milo mitatu (asubuhi, mchana na usiku).
“Vile vile baadhi ya kaya zimeweza kujijengea vijumba vidogo aina ya ‘slope’ na kuhama kwenye nyumba aina ya tembe. Kutokana na ruzuku ya masharti ya elimu na afya,mahudhurio ya watoto shuleni na kliniki, yamefikia zaidi ya asilimia 90,” alisema Dulle kwa kujiamini.
Katika hatua nyingine, mratibu huyo alisema pamoja na mafanikio hayo, bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ya baadhi ya walengwa hasa wa vijiji vilivyopo pembezoni kutokupata taarifa za tarehe za malipo kitendo kinachochangia washindwe kulipwa.
Alitaja changamoto nyingine kuwa ni baadhi ya walimu na waganga kudai kulipwa posho kwa kazi ya kujaza fomu za masharti ya elimu na afya. Kitendo hicho ni kinyume na maelekezo ya TASAF, kuwa kazi hiyo ni sehemu ya majukumu yao.
Dulle alitaja pia baadhi ya hatua za utatuzi wa changamoto hizo, kuwa ni watendaji wa vijiji wamehimizwa kuhakikisha walengwa wote wanajulishwa tarehe ya malipo siku mbili kabla.
“Walimu na waganga wamejulishwa kuwa ujazaji wa fomu za masharti,ni sehemu ya majukumu yao.Vijiji vimekumbushwa kuwa ujazaji wa fomu za mabadiliko ya taarifa za kaya,makazi na madai ya walengwa unafanyika kwa wakati,” alisema mratibu Dulle.

Post a Comment

 
Top