0
MASHIRIKA ya ndege nchini yametakiwa kupunguza gharama za usafiri wa anga ndani ya nchi ili kuweza kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje ya nchi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani alisema hayo jana wakati alipotembelea banda la wizara hiyo katika maonesho ya 40 ya kimataifa.
Alisema hatua hiyo ni mojawapo ya njia za kuhamasisha kuongezeka kwa watalii na kuchangia nusu ya fedha za kigeni tofauti na sasa wanapochangia robo ya fedha za kigeni.
Alisema nauli zipo juu hivyo ni wajibu wa mashirika ya ndege kuangalia upya viwango vinavyotozwa na kuvishusha, ili kuongeza watalii nchini.
Alisema mchakato wa mapitio ya nauli utasaidia kuongeza pato la taifa, ambapo kwa sasa sekta hiyo inaliongezea taifa asilimia 25 ya fedha za kigeni zitokanazo na utalii.
Makani alisema serikali inaendelea kuboresha barabara ndani ya hifadhi, viwanja vya ndege na kwingine ili kuwavutia watalii wanapokuja nchini.
Alisema wanakabiliana na changamoto ya kutangaza matangazo ya utalii ya kimataifa yatakayopokelewa na jumuiya ya kimataifa katika kuhamasisha utalii nchini.

Post a Comment

 
Top