0
WIZARA ya Maliasili na Utalii imetangaza punguzo kwa Watanzania watakaotembelea Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kwa watakaokwenda na kurudi na wale watakaolala katika hifadhi hizo.
Gharama hizo ni kwenda na kurudi kwa watoto itakuwa Sh 10,000 na watu wazima Sh 20,000 huku safari ya kulala itakuwa Sh 50,000.
Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari kutoka kwenye wizara hiyo ilisema punguzo hizo ni katika kipindi hiki cha Maonesho ya 40 ya Kimataifa ya Biashara yaliyofunguliwa rasmi jana na kufungwa Julai 8, mwaka huu.
Wizara hiyo pia ilisema itashirikiana na taasisi na idara za serikali 16 katika maonesho hayo ili kuongeza uelewa wa wananchi na kufahamu rasilimali zao zikiwemo idara hizo za utalii, wanyamapori, mambo ya kale na misitu na nyuki, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na Chuo cha Taifa cha Utalii.
Nyingine ni Makumbusho ya Taifa, Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (Tawiri) na Vyuo vya Wanyamapori (Mweka, Pasiansi na Likuyu Semaganga).
Taasisi nyingine ni vyuo vya misitu na nyuki (Olmotonyi, FITI Moshi na Chuo cha Nyuki Tabora), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Wakala wa Mbegu za Miti, Taasisi ya Utafiti wa Misitu na wadau wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa washiriki wote watakuwa kwenye banda moja la Maliasili, hivyo wizara inawakaribisha wananchi wote kwenye banda hilo ili waweze kujionea na kuelimika na mambo mbalimbali yanayohusu utalii, ufugaji wa nyuki, uhifadhi wa misitu, malikale na wanyamapori.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa katika maonesho hayo itakuwepo fursa ya kuwaona wanyamapori hai mbalimbali kama vile chui, nyoka, ndege wa aina mbalimbali pamoja na simba. Kaulimbiu ya Maonesho hayo mwaka huu inasema“Tunaunganisha Uzalishaji wa Masoko.”

Post a Comment

 
Top