0
KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL) imesema hadi kufikia Desemba mwaka huu itakuwa imeanzisha huduma ya mawasiliano ya simu za mkononi kupitia mfumo wa mawasiliano wa kisasa ili kuwawezesha wananchi kupata mawasiliano bora na ya uhakika.
Akizungumza kwenye viwanja vya Maonesho ya 40 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Ofisa Uhusiano wa TTCL, Edwin Mashasi alisema hatua hizo ni baadhi ya mageuzi makubwa yanayoendelea ndani ya kampuni hiyo, baada ya kupata umiliki wa hisa zake kwa asilimia 100.
Alisema hatua ya kuachana na mbia wake kampuni ya Airtel, hivi sasa TTCL imejipanga kuboresha huduma zake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mawasiliano kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya mkongo wa taifa wa mawasiliano ambao hutumia njia ya kisasa zaidi kuunganisha mawasiliano badala ya ule wa zamani unaotumia nyaya.
Akizungumzia mageuzi ya kampuni hiyo, Mashasi alisema hivi sasa wameingiza bidhaa mpya zinazotumia uwezo wa 4G LTE ambapo watumiaji wa vyombo vya mawasiliano vya data wanaweza kupata mawasiliano ya uhakika kupitia laini ya TTCL zilizounganishwa na masafa ya 4G.
Alisema hadi kufika Desemba mwaka huu kampuni hiyo itakuwa imeshaanza kutoa huduma ya mawasiliano ya simu za mkononi na kuwataka wananchi kuchangamkia huduma hiyo kwa sababu itakuwa nafuu na yenye kasi zaidi ukilinganisha na mitandao mingine ya simu za mkononi.

Post a Comment

 
Top