0
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG), Profesa Mussa Assad amesema kuwa fedha za serikali ni za wananchi hivyo zinapaswa kutumika kikamilifu na kwa malengo yaliyokusudiwa.
Assad aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati wa ufunguzi wa warsha ya usambazaji na ukusanyaji wa maoni ya ripoti ya CAG kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2014 kwa asasi zisizo za serikali.
Alisema kila taasisi ya umma inapaswa kutambua kuwa inawajibu wa kutumia fedha kikamilifu kwa kufuata taratibu na sheria zilizowekwa ili kuondoa ubadhirifu unaojitokeza.
“Ripoti yangu itasambazwa kwa wananchi na tayari imeshatafsiriwa kwa kiswahili hivyo kila mtanzania ataweza kusoma na kuona kilichoandikwa, ila napenda kurudia kuwa fedha za serikali ni za wananchi hivyo hazipaswi kutumika vibaya hata kidogo,” alisema.
Assad pia aliipongeza serikali kupitia programu ya maboresho yaani PFMRP pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo kama vile Shirika la Msaada la Marekani (USAID) kwa kuwawezesha kuwa na machapisho hayo.
Akizungumzia hali ya ukaguzi kwa mwaka uliopita, Assad alisema ilikuwa nzuri na kudai kuwa ofisi yake itaendelea kufanya kazi kama inavyotakiwa kwa kufuata taratibu na sheria.


Kwa upande wake Katibu Mkuu Chama cha Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Nicholaus Mgaya alisema ataisoma kwa kina ripoti hiyo iliyotafsiriwa ili iweze kugundua ni kwa nini baadhi ya halmashauri zinapata hati chafu na nini kifanyike.

Post a Comment

 
Top