0
BARABARA mpya zilizoongezwa katika mashindano ya mbio za magari za Oryx 2016 zimetajwa kuwa ni kipimo kizuri cha ustadi kwa madereva 25 watakaochuana Julai 9 na 10 kuwania taji la Afrika.
Barabara hizo zinazounganisha mji wa kihistoria wa Bagamoyo na vijiji vya Lugoba na Msata mkoani Pwani, zina urefu wa zaidi ya kilometa 200, ndiyo maeneo yenye umbali mrefu na changamoto nyingi kwa washiriki. Kwa mujibu wa Rais wa Chama cha Magari nchini, Nizar Jivani, washiriki hao wanatoka katika nchi sita za Afrika na Bara la Asia.
Waandaaji wa mbio hizo Automobile Association of Tanzania(AAT) walitangaza kuongeza sehemu tatu mpya za mbali na miji ili kuhamasisha ushindani na kuhakikisha usalama kwa washindani na watazamaji, kwa mujibu wa Jivani.
Miongoni mwa vivutio vikubwa ni njia inayopita katika ya mashamba ya mkonge ya Ubena Highland Estate, ambapo madereva watapata fursa ya kuiona taswira ya zamani ya Tanganyika, ambayo enzi zake mkonge ulikuwa ni zao maarufu.
Kichocheo kingine cha ushindani kwa mujibu wa waandaaji AAT ni kipande cha barabara kati ya Bagamoyo na Msata na Bagamoyo na Lugoba, ambayo hufuata njia iliyotumiwa zamani na watumwa.
“Mashindano haya pia yanajali maeneo muhimu ya kihistoria kama Kaole, ambako magari yatapita katika mzunguko wa pili Jumapili,” aliongeza Jivani.
Kwa mujibu wa waandaji,sehemu kubwa ya mashindano itafanyika mkoa wa Pwani wakati ni uanzishwaji tu wa mbio hizo utakaofanywa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ndiyo utafanyika jijini.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo ndiye atakeyefunga mashindano hayo mjini Bagamoyo.
Bingwa mtetezi mkongwe Gerald Miller wa Arusha ni mmoja wa madereva waliothibitisha kushiriki katika mashindano ya mbio za magari ya Oryx, ambayo ni raundi ya nne ya mbio za ubingwa wa magari barani Afrika.

Post a Comment

 
Top