0
TIMU ya Serengeti Boys leo inashuka dimbani ugenini kucheza na Shelisheli katika mchezo wa marudiano wa kusaka nafasi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17.
Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, Bakari Shime, alisema hatarajii kuwa na mabadiliko makubwa ya kikosi katika mchezo dhidi ya vijana Shelisheli utakaopigwa kesho Jumamosi Julai 2, 2016 kwenye Uwanja wa Stade Linite mjini Victoria.
“Timu haitakuwa na mabadiliko makubwa isipokuwa nitampumzisha Job (Dickson Nickson) tu katika mchezo wa kesho (leo), na nafasi yake atacheza Enrick (Vitalis Nkosi),” alisema Shime jana.
Shime alisema anauchukulia mchezo huo kwa uzito uleule na kuongeza ana sababu za kiufundi na kimbinu kumpumzisha Job katika mchezo wa marudiano kwani wana nafasi ya kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana, zitakazofanyika mwakani huko Madagascar.
Kwa hali halisi ilivyo timu iko vema na ikathibitishwa na Shime mwenyewe akisema: “Kikosi kiko vema kwa maana ya wachezaji wako vizuri na kambi iko vizuri kwa sababu hakuna majeruhi.” Pia Daktari wa timu hiyo, Shecky Francis Mngazija alithibitisha. “Sioni kama kuna dalili zozote za hujuma na kimbinu tumejipanga vema. Tumefuta matokeo ya Dar na tuko huku tunataka matokeo mapya. Mbinu zangu siku zote ni ushindi wa nyumbani na ugenini,” amesisitiza.
Serengeti Boys ilitua kwenye Kisiwa cha Mahe ulipo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Visiwa vya Shelisheli jana Juni 30, 2016 majira ya saa 11 jioni. Shime ana matumaini makubwa kuiondoa Shelisheli katika mbio hizo baada ya kuvuna ushindi mnono wa mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Jumapili ya Juni 26, 2016.
Na ili iweze kufuzu, Serengeti Boys inahitaji kusimama imara katika matokeo hayo ama kwa kupata sare ya aina yoyote, kushinda au ikitokea kupoteza, basi isifungwe zaidi ya mabao 2-0.
Katika mchezo wa Dar es Salaam waliozifumania nyavu walikuwa Nickson Kibabage, Ibrahim Abdallah na Ally Hussein ambaye alifunga kwa penalti na kila mmoja amepania kufunga kama kocha akiwapa nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza.

Post a Comment

 
Top