0
SERIKALI inajiandaa kufanya marekebisho ya Sheria ya Hifadhi ya Jamii ili kurejesha fao la kujitoa kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya baadhi ya sekta ambazo ajira zake ni za muda mfupi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu , Jenista Mhagama alisema hayo bungeni jana alipokuwa akijibu swali Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku maarufu Msukuma (CCM).
Msukuma katika swali lake alisema wafanyakazi katika migodi wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la kufukuzwa kazi ovyo, huku serikali ikiwa imeamua kufuta fao la kujitoa na kuhoji wafanyakazi hao wasubiri mpaka lini, ili wanufaike na mafao hayo wakati ni vijana?
Jenista alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano inataka kuwepo utaratibu wa kuwa na hifadhi ya jamii kwa wananchi wakati wa uzeeni na hivyo sheria iliyopo, ilitungwa kutekeleza matakwa ya Katiba.
Hata hivyo, utekelezaji wa matakwa hayo kwa mujibu wa Jenista, umeibua changamoto katika baadhi ya sekta za kiuchumi hasa madini na kilimo, ambazo wafanyakazi hufanya kazi za muda mfupi.
Kutokana na changamoto hiyo, Jenista alisema serikali inapitia upya sera na sheria ili zijibu matatizo ya wafanyakazi kwa kuzingatia aina ya kazi na sekta wanazotumikia na kuomba wafanyakazi, wawe na subira wakati mabadiliko ya sera na sheria hiyo yakifanyiwa kazi.
Alisema wanazo taarifa ya baadhi za kampuni, ambazo zina hati za mishahara mbili kwa kila mfanyakazi, moja ikionesha kima cha chini cha mshahara, ambayo ndiyo inayoonesha mchango wa mwajiri na mfanyakazi katika mifuko hiyo na kodi.

Post a Comment

 
Top