KAMPUNI ya Yono Auction Mart imeanza kuwaondoa kwa nguvu watu waliopanga na kununua nyumba za serikali ambao hawajamaliza kulipa madeni yao kwa wakati kama mikataba yao inavyoelekeza.
Kazi ya kuwaondoa watu hao ilianza jana katika eneo la Magomeni Usalama ambapo Chuo cha Zoom Polytechnic kilitolewa vyombo vyake nje kutokana na kudaiwa zaidi ya Sh milioni 44.
Akizungumza na gazei hili, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo ambayo imepewa kazi ya kukusanya madeni hayo, Scholastica Kevela alisema, wameanza na chuo hicho lakini kazi hiyo ni endelevu na itafanyika nchi nzima.
“Kwa leo (jana) tumeanza na Chuo cha Zoom ambacho kiko pale Magomeni Usalama, halafu tunarudi kujipanga na kesho (leo) tunaweza kuendelea kwa watu wengine ambao bado wanadaiwa,” alisema Kevela.
Aidha, Kevela alibainisha kuwa wapangaji na watu walionunua nyumba hizo ambao wanadaiwa wanatakiwa kutambua hata kama deni ni dogo kampuni hiyo haitakuwa na msalia Mtume bali itatoa vyombo nje na kupiga mnada nyumba hizo ili kulipa deni la serikali.
Aliongeza kuwa kwa wale watakaokuwa wanadaiwa madeni makubwa, kampuni hiyo itakamata vyombo na kuvipiga mnada ili kulipia deni wanalodaiwa. Aliwataka wote ambao hawajamaliza kulipa madeni yao watii sheria bila shuruti.
“Naomba kuwaambia wapangaji na walionunua nyumba za wakala wa Majengo, wajiandae kulipa kodi bila kufikiwa na mkono wa Yono,” aliongeza Kevela. Tayari kampuni hiyo inashikilia nyumba zaidi ya 50 kwani kuanzia juzi kampuni hiyo ilishikilia nyumba 20 Mwanza kwa kuwatoa watu nje na Dodoma nyumba 40 zikiwemo za vigogo.
Alisema TBA imewapa orodha ya nyumba zaidi ya 3,000 nchi nzima za walionunua na wengine kupangisha za TBA ambao wanadaiwa na muda wa kulipa madeni yao ulishapita.
Post a Comment