RAIS John Magufuli (pichani) amesema Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kumaliza makosa yote yaliyojitokeza huko nyuma ikiwemo tatizo la watumishi na wanafunzi hewa lililoibuka hivi karibuni.
Amewataka Watanzania kuacha kuingiza siasa kwenye makosa yanapojitokeza, hasa yale yanayogusa sehemu nyeti kama elimu, kwani yakiachwa kuna uwezekano wa kutengeneza taifa la watu wa ajabu.
Alisema tangu aingie madarakani amekumbana na changamoto mbalimbali, ikiwemo matatizo ya rushwa, ukwepaji kodi, watumishi hewa na sasa amekumbana na tatizo la wanafunzi hewa.
“Nchi yetu ina changamoto na mambo mengi sana hata mimi nimekumbana na changamoto naziona mwenyewe, nikigeuka hivi watumishi hewa ambao hadi sasa wamefikia 10,500, nikigeuka hivi kuna wanafunzi hewa,” alisisitiza.
Alisema ni Tanzania pekee ambayo mtu anaweza kupata daraja la nne kidato cha nne katika elimu ya sekondari, halafu akapata fursa ya kujiunga na chuo kikuu na kupatiwa mkopo wa serikali, wakati mhitimu aliyefaulu kidato cha sita akikosa fursa hiyo.
Alisema endapo kulifanyika makosa lazima yarekebishwe, kwani inafahamika fika mtu akimaliza kidato cha nne akifeli ataanzia ngazi ya Astashahada, Stashahada ndio apate nafasi ya kujiunga chuo kikuu.
“Sasa hapa kwetu ni tofauti ukifeli kidato cha nne unajiunga chuo kikuu,” alihoji na kuwataka watu waache siasa kwenye makosa kwani mambo kama hayo yakiachwa kuna hatari ya nchi kutengeneza taifa la ajabu.
Hivi karibuni, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako aliivunja Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na kuwasimamisha kazi viongozi wanne waandamizi kwa tuhuma za kudahili wanafunzi wasio na sifa.
Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya TCU, Awadh Mawenya naye alisimamishwa kazi kwa kosa la kushindwa kuwachukulia hatua watumishi waliodahili wanafunzi hao wasio na sifa. Profesa Ndalichako alichukua hatua hizo baada ya TCU kudahili wanafunzi 489 waliopata daraja la 4.32 katika mitihani yao ya kidato cha nne lakini walijiunga na chuo kikuu na kupatiwa mikopo yenye thamani ya Sh milioni 784.
Post a Comment