POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imesema ingawa imepokea barua kutoka kwa wakili wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, Peter Kibatala ikieleza kuwa amesafiri, wamemtaka afike katika kituo hicho atakaporudi kutoka safarini.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu, Simon Sirro alisema wakati wakiendelea kumtafuta Gwajima, wamepokea barua kuwa amesafiri na anatarajia kurejea nchini kabla ya Julai mosi na pindi atakaporejea nchini atakwenda kuripoti Polisi.
“Sisi kwa sasa tunaendelea kumsubiri ili tumhoji,” alisema Sirro. Kwa mujibu wa taarifa zilizotoka katika vyombo vya habari, wakili wa Askofu huyo alitoa taarifa kuwa yuko nje ya nchi na kabla hajasafiri hakuwa amepata taarifa rasmi kuhusu kutakiwa kwake Polisi.
Wakili huyo alimuandikia barua Sirro akisema kuwa mteja wake alitaka amtaarifu kuwa akisharejea nchini atakwenda kuripoti katika kituo hicho haraka iwezekanavyo. Askofu Gwajima anatafutwa na jeshi hilo ili ahojiwe juu ya mahubiri yake aliyoyatoa Juni 11, mwaka huu kanisani kwake Ubungo Maji jijini Dar es Salaam.
Katika mahubiri hayo yaliyosambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii, Gwajima alisikika akiukosoa utendaji kazi wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Post a Comment