0
WAJASIRIAMALI nchini wanaofanya biashara mbalimbali kwa njia ya mtandao, wametakiwa kutumia vyema fursa itokanayo na Teknolojia ya Mawasiliano katika kukuza biashara zao.
Mwito huo umetolewa jana na Mkuu wa Huduma za Kifedha wa Kampuni ya simu za mkononi ya Tigo, Ruan Swanepoel wakati wa uzinduzi wa huduma mpya ya kampuni hiyo inayolenga kuwawezesha wajasiriamali wa mitandaoni kutengeneza huduma za kutangaza bidhaa kirahisi zaidi ijulikanayo kama API.
Swanepoel alisema kupitia huduma yao hiyo mpya, vijana wanaojishughulisha na ujasiriamali kwa njia ya mitandao, wanaweza kujitengenezea mfumo wa kutangaza bidhaa zao kirahisi kwa kutumia huduma hiyo ya API.
Alisema wanaweza kuipakua huduma hiyo katika simu zao au kwa kuingia katika tovuti ya Tigo, kisha kuanza kutoa huduma hiyo.
Alisema vijana iwapo wakitumia API wanaweza kukuza biashara zao, kwa kuwa watakuwa wamejiweka katika mazingira mazuri ya kutangaza bidhaa zao mbalimbali kwa njia ya mitandao.
“Kwa sasa vijana wengi nchini wamekuwa wakijikita zaidi katika nyanja ya teknolojia na wamekuwa wakitumia fursa mbalimbali katika kujitangaza, sasa Tigo imewasogelea karibu zaidi kwa kuwawekea mfumo ambao unawawezesha kufanikisha lengo lao hilo kirahisi,” alisema.

Post a Comment

 
Top