0

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohammed Abood.

WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wameitaka Serikali kuchukua hatua za kisheria kupambana na watu wanaofanya vitendo vya hujuma ikiwemo kushawishi wananchi na wafanyabiashara wasilipe kodi.
Hayo yalisemwa na Mjumbe wa Kamati ya Wenyeviti ya Baraza la Wawakilishi, Machano Othman Said wakati akisoma maoni ya kamati hiyo kwa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017. Said alisema hivi sasa wapo viongozi wanaopita kila kona kuwashawishi wafanyabiashara wasilipe kodi kwa sababu tu za kisiasa.
Alisema tabia hiyo haiwezi kuvumiliwa hata kidogo kwa sababu kitendo cha kushawishi wafanyabiashara wasilipe kodi ni sawa na kurudisha nyuma maendeleo ya nchi ambayo yanategemea sana makusanyo ya kodi kutoka kwa wafanyabiashara.
Akichangia bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/2017 aliitaka Serikali kulishughulikia tatizo la mgomo wa wafanyabiashara ikiwemo kupandisha bei kwa makusudi. Aidha, aliitaka Serikali kuacha kuwafumbia macho viongozi wanaoshawishi wananchi na wafanyabiashara wasilipe kodi na kutaka kuwachukulia hatua za kisheria.
“Mfanyabiashara ambaye anagoma kulipa kodi sheria zipo wazi ni kufuta leseni ya biashara kwa sababu amekwenda kinyume na sheria na masharti ya biashara,” alisema kwa hisia kali.
Mwakilishi wa Jimbo la Uzini, Mohammed Raza Dharamsi aliwataka wafanyabiashara kuendelea kushirikiana na Serikali kwa ajili ya kuleta bidhaa mbalimbali za vyakula kwa wingi katika kipindi kinachokaribia cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Alisema hadi sasa hakuna sababu zinazowafanya wafanyabiashara kupandisha bei ya bidhaa zao kwa sababu hakuna ongezeko la aina yoyote ya kodi.

Post a Comment

 
Top