0
Mufti wa Tanzania, Shekhe Abubakar Zuberi Ally.

MASHEHE na wanazuoni wametakiwa kufanya tafiti mbalimbali na kuandika katika vitabu au vipeperushi ili vitumiwe na vizazi vijavyo. Pia, vijana nchini wametakiwa kuwa na tabia ya kusoma vitabu vya dini kwani vitasaidia kuwaondoa katika matatizo yanayowakabili, ikiwamo utumiaji wa dawa za kulevya.
Mwito huo umetolewa jijini Dar es Salaam jana na Kiongozi Mkuu wa Chuo cha Kiislamu cha Imam Swadiq na Shehe Mkuu wa madhehebu ya Shia, Hemed Jalala wakati wa uzinduzi wa Maktaba yenye vitabu mbalimbali vya dini.
Shehe Jalala alisema vijana wengi wanapitia matatizo mbalimbali kutokana na kutokusoma maandiko matakatifu, kama vile Biblia na Quran. ‘’Tumezindua Maktaba hii kwa lengo la kutoa nafasi kwa vijana wetu kubadili mienendo yao ya kimaisha na kuenenda katika njia zilizo sahihi za kumpendeza Mungu,’’ alisema.
Pia alisema kupitia maktaba hiyo, vijana wa dini zote watajitambua kwamba wao ni nguvu kazi ya Taifa inayotegemewa katika kuleta maendeleo katika nchi. Alisema kuwa mashehe na maimam ambao hawaandiki makala, vitabu na vipepeshi ni mzigo kwa sababu hawaendani na wakati uliopo.
‘’Si vyema kuona Imam, Shehe ambao hawaandiki makala na kuzichapisha kwenye vipeperushi, mitandao ya kijamii na magazeti. Hii ni dalili kuwa shehe huyo hana jipya na haendani na wakati,’’ alisema Shehe Jalala.

Post a Comment

 
Top