Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) nchini Tanzania imezindua huduma mpya katika juhudi za kuimarisha vita dhidi ya rushwa nchini humo.
Kupitia huduma hiyo iliyopewa jina Longa Nasi, wananchi wataweza kutoa taarifa kuhusu visa vya ulaji rushwa kupitia simu za mkononi.
Anayetoa taarifa anaweza kuwapasha maafisa kwa kupiga simu au kwa kutuma ujumbe mfupi kwa nambari maalum.
Huduma hiyo inatumika katika mitandao yote ya simu bila malipo.
Rais wa Tanzania John Magufuli aliahidi kukabiliana vikali na ulaji rushwa wakati wa kampeni na amekuwa akiwafuta kazi baadhi ya maafisa wakuu serikalini kwa tuhuma za kuhusika au kutozuia ufisadi.Desemba mwaka jana, alitengua uteuzi wa mkuu wa Takururu Dkt Edward Hoseah kutokana na “kutoridhishwa na namna taasisi hiyo ilivyokua ikitekeleza wajibu wake katika kukabiliana na rushwa hususani kwenye upotevu wa mapato ya serikali katika bandari ya Dar es salaam.”
Dkt Magufuli amesifiwa na baadhi ya mashirika na viongozi kutoka nje kwa juhudi zake kukabiliana na rushwa.
Majuzi, Dkt Magufuli alipohudhuria sherehe ya kuapidhwa kwa Rais wa Uganda Yoweri Museveni, kiongozi huyo wa Uganda alisema hatua zake zimerahisisha shughuli mpakani .
"Napenda kasi yako ya uongozi, napenda jinsi unavyopambana na rushwa, kwa sababu rushwa ilikuwa inazaa matatizo mengine kama vile ucheleweshaji wa mizigo bandarini na vikwazo vya mpakani, hivyo nakupongeza sana kwa hilo,” alisema Bw Museveni
Post a Comment