Polisi nchini Tanzania wanawazuilia watu watatu wanaotuhumiwa kuhusika shambulio katika msikiti mmoja mjini Mwanza magharibi mwa nchi hiyo.
Watu watatu, akiwemo Imam, walifariki wakati wa shambulio hilo lililotekelezwa katika msikiti wa Rahman wakati wa swala ya usiku siku ya Jumatano.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi jijini humo, Ahmed Msangi, uchunguzi wa mwanzo umebaini kwamba mauaji hayo yalifanywa kwa kutumia mapanga na kuongeza kuwa, polisi wanachunguza chanzo cha shambulizi hilo.
Baadhi ya walioshuhudia tukio hilo, wamesema shambulio hilo lilitekelezwa na kundi la watu wasiopungua 15.
Hakuna aliyedai kuhusika katika shambulio hilo.
Tukio jingine la mauaji ya kutumia silaha pia limetokea katika mkoa wa Pwani wilaya ya Mkuranga ambapo askari polisi aliyefahamika kwa jina la Sajenti Kinyogoli ameuawa na watu wasiojulikana.
Matukio hayo yote yametokea wiki hii kulipoibuka taarifa kwenye mtandao wa Twitter juu ya kikundi kilichojitambulisha kama wafuasi wa mtandao wa kigaidi wa Islamic State wakifanya mazoezi eneo la Tanga, kaskazini mashariki mwa Tanzania.
Post a Comment