SERIKALI jana ilitoa majibu mapya yenye ufafanuzi wa kina kwa swali lililojibiwa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga ambalo pamoja na masuala mengine, limeeleza mkakati wa serikali kujenga nyumba zaidi ya 9,000 kwa ajili ya askari Magereza na Polisi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alijibu swali hilo jana lililoulizwa na Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema) kwa niaba ya Mbunge wa Viti Maalumu, Devotha Minja (Chadema).
Akiuliza, Selasini alisema, “Sasa naomba swali namba 211 la Mheshimiwa Devotha Minja lililoleta kasheshe sasa lijibiwe.” Hata hivyo swali lililosababisha uteuzi wa Kitwanga kutenguliwa Ijumaa iliyopita, liliulizwa na Mbunge wa Mlimba, Suzan Kiwanga kwa niaba ya Minja kuhusu serikali kuwaboreshea askari makazi, ambalo hata hivyo ilibainika Waziri alikuwa amelewa.
Baada ya majibu ya Waziri Kitwanga, jioni yake, Rais John Magufuli alitangaza kumfuta kazi Kitwanga kwa kosa la kujibu swali akiwa amelewa. Baadaye Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema) aliomba Mwongozo wa Spika akisema halikujibiwa kikamilifu kama kanuni zinavyoelekeza. Baadaye jioni, Kiti cha Spika kilijibu mwongozo huo na kuamuru kuwa swali hilo lijibiwe kikamilifu Jumatatu (jana).
Nyumba za Magereza, Polisi Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alisema katika kukabiliana na tatizo hilo la makazi kwa askari, serikali imeendelea na mpango wa kuzifanyia ukarabati mkubwa baadhi ya nyumba kwenye baadhi ya Magereza na kujenga nyumba mpya.
“Mahitaji ya nyumba hivi sasa ni nyumba 14,500 wakati zilizopo ni 4,221 hivyo kuwepo upungufu wa nyumba 10,279 ambao unalazimisha baadhi ya askari kuishi nje ya kambi za Jeshi la Magereza,” alisema Masauni.
Alisema serikali kupitia Jeshi la Magereza, imesaini mkataba na Kampuni ya Poly Technologies ya China kwa kujenga nyumba 5,900 kwenye vituo vyote vya magereza nchini. Aliutaja mgawanyo wa ujenzi wa nyumba hizo ni Makao Makuu ya Magereza nyumba 472, Arusha 377, Dar es Salaam 952, Dodoma 356, Kagera 364, Kigoma 272, Kilimanjaro 290 na Lindi 233.
Nyingine ni Manyara 206, Mara 378, Mbeya 622, Iringa 622, Iringa 336, Morogoro 369, Mtwara 215, Mwanza 398, Pwani 384, Rukwa 358, Ruvuma 320, Shinyanga 337, Singida 299, Tabora 408, Tanga 382 na KMKGM Dar es Salaam 219.
Aidha, Chuo cha Ukonga 115, Chuo cha Kiwira 183, Chuo Ruanda 62, Chuo KPF 27, Bohari Kuu 82 na Bwawani 84. Akizungumzia Jeshi la Polisi, alisema serikali inakusudia kujenga nyumba 4,136 katika mikoa 19 ya Tanzania Bara na Zanzibar.
“Serikali itaendelea kutatua changamoto ya uhaba wa nyumba kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo mikopo yenye riba nafuu, miradi Shirikishi (PPP) na kwa kutumia fedha za bajeti ya serikali kadri hali ya uchumi itakavyokuwa ikiimarika,” alisema Masauni.
Akijibu maswali ya nyongeza ya Selasini, Naibu Waziri alisema si kweli kuwa magereza yameacha shughuli za uzalishaji uchumi kama kilimo, ushonaji na ufugaji. Alisema jeshi hilo lina mpango kabambe wa kuendesha miradi hiyo na imeshaandika andiko la miradi minane lililowasilishwa serikalini na pia tayari wameandaa mpango kazi wa kujitegemea.
Alitaja miradi hiyo kuwa ni ya kilimo, ushonaji viatu, samani, umwagiliaji, ufugaji ng’ombe, ulimaji alizeti na mpunga katika magereza yakiwamo ya Kigongoni, Karanga, na Songwe.
Post a Comment