0
Jimbo moja nchini Nigeria limetangaza hali ya hatari kutokana na uhaba mkubwa wa nyanya.
Jimbo hilo la Kaduna, kaskazini mwa Nigeria, limechukua hatua hiyo baada ya wadudu waharibifu wajulikanao kama Tomato Leaf Miner au Tuta Absoluta kuharibu nyanya mashambani.
Kamishna wa Kilimo katika jimbo hilo Daniel Manzo Maigar amesema wadudu hao wameharibu 80% ya nyanya katika jimbo hilo.
Amesema wakulima 200 wamepata hasara ya zaidi ya naira bilioni moja ($5.1m; £3.5m) katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita.
Bei ya nyanya kikapu kimoja imepanda kutoka $1.20 chini ya miezi mitatu iliyopita hadi zaidi ya $40.
Mwandishi wa BBC aliyepo Nigeria Muhammad Kabir Muhammad anasema maafisa katika jimbo hilo wametangaza hali ya hatari kuonesha wanachukua hatua kutatua tatizo hilo.
Serikali ya jimbo hilo pia imewatuma maafisa wake wa kilimo Kenya kukutana na wataalamu kuhusu Tomato Leaf Miner kufahamu zaidi jinsi ya kukabiliana na wadudu hao.
Kaduna hupatikana kaskazini mwa Nigeria na kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, ndipo ukuzaji wa nyanya hufanywa kwa wingi.
nyanya
Image captionWadudu waharibifu wameharibu nyanya zikiwa mashambani
Mapema mwezi huu, kampuni ya kutengeneza nyanya za kupondwa na kuwekwa kwenye mikebe inayomilikiwa na Aliko Dangote, ilisitisha shughuli zake kutokana na uhaba wa nyanya, kwa mujibu wa Forbes.
Nyanya hutumiwa sana katika vyakula Nigeria na ‘tomato’, jina la nyanya kwa Kiingereza, limekuwa likivuma sana katika Twitter nchini humo watu wakijadili kupanda kwa bei.
Moja ni kibonzo cha Mnigeria akiwa ameshangaa baada ya kugundua kuna tamasha linalofanyika Uhispania ambapo watu hurushiana nyanya.

Post a Comment

 
Top