0

Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani.

WIZARA ya Uchukuzi na Mawasiliano imesema hakuna kiwango kinachobainisha wazi kuwa ndege yenye uwezo wa kubeba abiria 10 au zaidi ni sharti iendeshwe na marubani wawili, imeelezwa.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani alitoa ufafanuzi huo jana bungeni na kusema, hakuna hata mapendekezo ya kiutekelezaji kwenye suala hilo. Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Mtambwe, Khalifa Mohamed Issa (Cuf) aliyehoji serikali haioni kuruhusu ndege kuongozwa na rubani mmoja ni sawa na kuweka rehani maisha ya abiria, na sheria inasemaje kuhusu ndege ya abiria kurushwa na rubani mmoja.
Ngonyani alisema taratibu zinazoongoza fani ya kuendesha ndege nchini huongozwa na miongozo inayokubalika kimataifa ambayo imeridhiwa nchini. Alisema marubani hupimwa afya zao na madaktari bingwa kila muda kulingana na umri kama ilivyoainishwa katika Kanuni ya 140 hadi 177 ya Kanuni za Usafiri wa Anga (Leseni binafsi).
“Serikali huruhusu ndege kuendeshwa na rubani mmoja kwa kuzingatia taratibu hizo,” alisema Naibu Waziri. Alisema ndege iliyoandikishwa Tanzania na kuruka kwa shughuli za kibiashara yenye uzito unaozidi kilo 5,700 itakuwa na marubani wasiopungua wawili.
Alisema shughuli za usalama wa anga nchini zinaongozwa na Sheria Namba 80 na Kanuni zilizotengenezwa chini yake. Alisema urushaji wa ndege yenye abiria tisa au zaidi unaongozwa na Kanuni ambayo ndege inayotimiza vigezo vilivyowekwa kuwa na uzito wa kilo 5,700 inaruhusu kuendeshwa na rubani mmoja.

Post a Comment

 
Top