MHE UMMY MWALIMU
KARANI wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU), Bakari Mlanga (23) amehukumiwa miaka 27 jela huku Ahmed Mbinjika (25) atatumikia kifungo cha miaka 12 baada ya kupatikana na hatia ya kughushi fomu za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Washtakiwa hao walihukumiwa kifungo hicho jana katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Juma Hassan. Hakimu Hassan alisema upande wa mashitaka, ulileta mashahidi watano kuthibitisha mashitaka hayo na kwamba Mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.
Alisema kuwa mshtakiwa Mlanga amekutwa na hatia katika makosa tisa, ambapo kwa kila kosa kwa makosa manane, atatumikia miaka mitatu na kosa la tisa kutumikia kifungo cha miezi 12. Pia alisema Mbinjika amekutwa na hatia kwa makosa manne, ambayo kila kosa atatakiwa kutumikia kifungo cha miaka mitatu.
Alisema kupitia mashahidi, washtakiwa walighushi fomu hizo kuchukulia dawa za kisukari na shinikizo la damu katika maduka mbalimbali yaliyopo jijini Dar es Salaam. Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Florida Wenslaus aliiomba Mahakama kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria, iwe fundisho kwao na wengine wenye tabia kama hizo.
Katika mashitaka yao, ilidaiwa kuwa Desemba 15, 2014 washtakiwa walighushi fomu ya NHIF ya Tito Mfilinge, kuonesha kuwa imesainiwa na Dk Emma Chambenga kuonesha kwamba ni halali kutumika.
Pia ilidaiwa katika tarehe hiyo hiyo, walighushi fomu ya NHIF ya kuchukulia dawa ya Felister Msendekwa iliyoandikwa Desemba 9, 2014 na kuonesha kuwa ilisainiwa na daktari huyo na walifanya makosa hayo mara nyingi kwa nyakati tofauti.
Post a Comment