0
Simu iliyotumiwa na Adolf Hitler wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia imeuzwa kwa $243,000 (£195,744) katika mnada Marekani.
Maelezo kuhusu aliyeinunua, ambaye aliwasilisha ombi lake la ununuzi kupitia simu, hayajatolewa.
Mnada huo ulifanyika katika jiji la Chesapeake, Maryland, na bei ya chini kabisa ilikuwa $100,000.
Simu hiyo nyekundu, ambayo imechongwa jina la kiongozi huyo wa Nazi, ilipatikana katika handaki alimokuwa anajificha Hitler wakati mmoja mjini Berlin mwaka 1945.
Wanajeshi wa muungano wa Usovieti waliikabidhi simu hiyo kwa mwanajeshi Mwingereza Sir Ralph Rayner kama zawani muda mfupi baada ya Ujerumani kusalimu amri na kukubali kushindwa katika vita hivyo.
Mnada huo uliongozwa na wapiga mnada wa Alexander Historical Auctions.
Maafisa wa wapiga mnada hao wanasema simu hiyo ilikuwa kama "silaha ya maangamizi makubwa", kwani ilitumiwa na Hitler kutoa maagizo yaliyopelekea kuuawa kwa watu wengi wakati wa vita hivyo.
Sanamu ya kauri ya mbwa aina ya Alsatian, aliyemilikiwa na Hitler, pia iliuzwa katika mnada huo kwa jumla ya $24,300. Ilinunuliwa na mtu tofauti na aliyenunua simu.

Post a Comment

 
Top