Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, kiongozi wa taifa mwenye umri wa juu zaidi duniani kwa sasa, ametimiza miaka 93.
Kiongozi huyo anatarajiwa kujumuika kwa sherehe ya faradha na jamaa, wafanyakazi wake wa karibu na baadhi ya maafisa wakuu serikali.
Sherehe kubwa rasmi, inayotarajiwa kugharimu zaidi ya dola milioni moja za Kimarekani, itaandaliwa siku ya Jumamosi.
Rais Mugabe aliongoza Zimbabwe kupata uhuru wake mwaka 1980 na ametangaza kwamba anapanga kuwania katika uchaguzi mkuu mwaka ujao, ambapo atakuwa na umri wa miaka 94.
Mugabe alizaliwa 21 Februari, 1924.
Alifungwa jela 1964-1974 kwa kutoa "hotuba ya kuhujumu serikali"
Baada ya kuachiliwa, alisaidia kuongoza vita dhidi ya serikali ya Rhodesia
Vita vilipomalizika, Mugabe alishinda uchaguzi 1980 na akawa waziri mkuu wa Zimbabwe na akaongoza taifa hilo kama waziri mkuu hadi mwaka 1987.
Anaposherehekea kutimiza miaka 93, Umoja wa Ulaya umepiga kura kuongeza vikwazo dhidi yake.
Vikwazo hizo vinahusu usafiri, kuzuiliwa kwa mali yake na kupiga marufuku biashara ya silaha baina ya mataifa wanachama wa EU na Rais Mugabe, mkewe na wizara ya ulinzi ya Zimbabwe.
Hata hivyo, baraza la EU lilipiga kura kuondoa sehemu ya marufuku ya ununuzi wa silaha dhidi ya Zimbabwe.
Umoja huo sasa utaruhusu taifa hilo kuagiza kutoka nje vilipuzi ambavyo vinatumiwa katika uchimbaji wa madini na ujenzi wa miundo mbinu.
Vikwazo hivyo vitatathminiwa upya mwaka ujao.
EU ilimuwekea Mugabe vikwazo mara ya kwanza mwaka 2002 baada ya kuvamiwa kwa mashamba yaliyomilikiwa na Wazungu pamoja na tuhuma za wizi wa kura uchaguzini na ghasia na dhuluma dhidi ya upinzani na watetezi wa haki za kibinadamu.
Rais Mugabe anasema vikwazo hivyo vimesababisha madhila yasiyo na kifani kwa nchi yake, na kwamba ni sehemu ya mpango wa Uingereza kutaka kumuondoa madarakani.
Post a Comment