Ofisi ya mashitaka ya Rwanda
imetangaza kuanza upelelezi kuhusu askari 20 wa nchi ya Ufaransa katika
mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Katika tangazo hilo Rwanda inasema kuwa imeanza rasmi mchakato wa kisheria kuhusu maafisa hao wanaotuhumiwa hukusika moja kwa moja katika mauaji ya kimbari.
Mwendesha mashitaka mkuu wa Rwanda Richard Muhumuza alimwandikia mwezake wa Ufaransa Jean Claude Marin kutaka ushirikiano wa kisheria kuwasaidia wapelelezi wa Rwanda kuwahoji maafisa hao wa Ufaransa kupitia ubalozi wa Rwanda mjini Paris.
Maafisa hao 20 ni miongoni mwa askari wa Ufaransa waliokuwa katika kazi mbali mbali nchini Rwanda kuanzia mwaka 1990 hadi mwaka 1994.
Rwanda inawatuhumu kulisaidia jeshi la rais wa zamani Juvenal Habyarimana kwa silaha na kutoa mafunzo kwa wanamgambo wa Interahamwe waliotekeleza mauaji ya kimbari.
Tangazo hilo linasema kwamba wakati wa upelelezi huo pia baadhi ya viongozi wengine au wajumbe wa serikali ya Ufaransa wanaweza kuombwa kutoa taarifa zinazoweza kusaidia mwendesha mashitaka.
Orodha ya maafisa hao 20 ilifanywa kwa kuzingatia ripoti mbali mbali zilizofanywa kuhusu nafasi ya Ufaransa katika mauaji ya kimbari.
Rwanda ilivunja uhusiano wake na Ufaransa mwaka 2006 baada ya jaji wa Ufaransa kutoa waranti za kuwakamata maafisa 10 wa jeshi la Rwanda kwa tuhuma za kudungua ndege ya rais wa zamani wa Rwanda Juvenal Habyarimana,tukio ambalo linadaiwa kuwa chanzo cha mauaji ya kimbari.
Hata hivyo ziara ya aliyekuwa rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy nchini Rwanda mwaka 2010 ilirejesha matumaini ya uhusiano mpya.
Hakuomba msamaha kwa niaba ya taifa lake lakini alikiri kuwepo makosa ya kisiasa yaliyofanywa na baadhi ya viongozi wa nchi yake ambayo hata hivyo hakufafanua.
Hivi karibuni Ufaransa ilitangaza hatua ya kurejelea upya upelelezi kuhusu aliyedungua ndege ya rais wa zamani wa Rwanda Juvenal Habyarimana kwa kumhusisha mkuu wa zamani wa jeshi ya Rwanda jenerali Kayumba Nyamwasa ambaye sasa ni mpinzani mkuu wa rais Kagame.
Hatua hii imekasirisha sana Serikali ya Rwanda ambapo Rais Paul Kagame alisema kuanza upya upelelezi huo ni kitendo cha uchokozi dhidi ya nchi yake baada ya upelelezi wa awali uliofanywa na Ufaransa yenyewe kubainisha kuwa ndege hiyo ilidunguliwa na wafwasi wakereketwa wa hayati Habyarimana;na kwamba nchi yake iko tayari kupigania hadhi yake.
Post a Comment