0
Serikali ya Marekani imetangaza kwamba itazuilia mali ya maafisa wawili wakuu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Marekani inawatuhumu wawili hao, mkuu wa zamani wa polisi Jenerali John Numbi na afisa mkuu wa jeshi Meja Jenerali Gabriel Amisi ajulikanaye kwa majina ya utani kama Tango Fort au Tango Four kwa kuwa "tishio kwa uthabiti na kuhujumu shughuli za kidemokrasia".
Wizara ya fedha ya Marekani imesema hatua hiyo imechukuliwa kufuatia kuzidi kwa vitendo vya ukandamizaji dhidi ya wapinzani, sana kwa kutumia nguvu.
Kwa mujibu wa kituo cha redio cha Virunga Business, ingawa Jenerali Amisi bado anahudumu, John Numbi hajatekeleza majukumu rasmi kwa miaka mingi tangu kuuawa kwa mtetezi wa haki za kibinadamu Floribert Chebeya. Jenerali Numbi alisimamishwa kazi Juni 2010 baada ya kifo cha mwanaharakati huyo.
"Maafisa hawa wa serikali ya DR Congo wamejihusisha katika vitendo vya kuhudumu shughuli za kidemokrasia na kukandamiza haki za kisiasa na uhuru wa watu wa Congo, na kuzidisha hatari ya kuenea kwa ukosefu wa uthabiti DR Congo na eneo lote la Maziwa Makuu," kaimu mkurugenzi wa idara inayoangazia mali ya raia wa nje ya Marekani John Smith amesema kupitia taarifa.
Miezi minne iliyopita, mkuu wa polisi wa Kinshasa Celestin Kanyama pia aliwekewa vikwazo.
Bw Numbi anatoka Kolwezi, mkoa wa Katanga na anadaiwa kutumia nguvu na kuwatisha wapinzani wakati wa uchaguzi wa majimbo uliofanyika Machi 2016.
Anadaiwa kutishia kuua wapinzani wa wagombea wanaomuunga mkono Rais Joseph Kabila iwapo hawangejiondoa. Wagombea watatu wanadaiwa kujiondoa kutokana na vitisho hivyo.
"Ingawa si afisa wa serikali ya DR Congo tena, Numbi bado anaaminika kuwa mshauri wa Rais Kabila mwenye ushawishi mkuu," taarifa ya Marekani imesema.
AmisiImage copyrightAFP
Image captionJenerali Amisi, ajulikanaye pia kama Tango Fort
Jenerali Amisi anadaiwa kuwa kiongozi wa kundi la kijeshi linalosimamia mikoa ya Bandudu, Bas Congo, Equateur na Kinshasa, ambao walitumiwa kuzima maandamano ya kisiasa, hasa yaliyoandaliwa na upinzani na mashirika ya kiraia Januari 2015.

Post a Comment

 
Top