0
KATIBU Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit amesema kuwa, maofisa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) waliwahujumu katika mchezo wao dhidi ya TP Mazembe ya Congo DR.
Yanga walifungwa bao 1-0 na TP Mazembe katika mchezo wa Kundi A wa Kombe la Shirikisho uliofanyika Jumanne kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam. Alisema kuwa msimamizi wa Shirikisho la Soka Afrika, CAF, Jerome aliwaambia kuwa viongozi wa TFF walitaka mchezo huo ufutiliwe mbali.
Alisema hata Jerome alishangaa kwa nini TFF walitaka mchezo huo ufutwe, badala ya kuungana na wawakilishi wao (Yanga) kuhakikisha mchezo huo unafanyika kwa mafanikio.
“Hakukuwa na makubaliano kuhusu kuingia watazamaji 40,000, Malinzi kapotoshwa, kwani msimamizi aliuliza tunatarajia watu wangapi wataingia katika mchezo huo na mimi nilimjibu kwa kuwa ni bure, tunatarajia watu 60,000 na aliandika. “Suala la ulinzi hatukurupuka, kwani tulizungumza na Sirro (Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam) alituhakikishia usalama, hata hivyo tunaomba radhi kwa kadhia iliyotokea na siku zijazo ikitokea mchezo bure tutaboresha isitokee tena.”
Alisema kuwa wanashirikiana na serikali kuhakikisha wanafanya tathmini ili kujua uharibifu uliofanywa Uwanja wa Taifa ili waweze kulipa gharama zote. Alisema kuwa eti TFF inasema inashirikiana na sisi (Yanga) kuhakikisha tunasonga mbele, hiyo haina ukweli kabisa kwani lengo lao ni kutukandamiza hadi mjumbe huyo wa Caf anashangaa.
Naye msemaji wa klabu hiyo, Jerry Muro alisema jana kuwa ataiburuza mahakamani TFF kwa kuwa wamemkosea na kumuumiza kisaikolojia mara kwa mara.
“Malinzi na Mwesigwa (Katibu mkuu wa TFF), waniombe radhi kabla ya kesho (leo saa 4), sivyo nitawapeleka katika mahakama za kiraia".
Alisema kuwa barua imetumwa kwa Jerry binafsi wakati yeye ni msemaji wa Yanga na yuko pale kwa niaba ya klabu hiyo na sio yeye binafsi. Alisema barua hiyo imemuumiza kisaikolojia na tayari ana jopo la wanasheria wake, ambao wako tayari kuiburuza TFF mahakamani.

Post a Comment

 
Top