Polisi nchini Zambia wamewakamata watu 28 baada ya kuwarushia mabomu ya kutoa machozi katika maakazi ya mwanasiasa mmoja wa upinzani Goffrey Bwalya Mwamba.
Maafisa hao wanasema walikuwa wanatafuta watu walioharibu picha za kampeni ya uchaguzi na kisha wakatorokea kwenye makaazi hayo yaliyoko kazkazini mwa nchi hiyo.
Afisa mmoja wa polisi amesema mabomu ya petroli pia yalipatikana kwenye maeneo hayo lakini Bw. Mwamba amesema ni polisi ndio waliotegesha mabomu hayo na kisha kumsingizia yeye.
Kumekuwa na wasiwasi kwamba huenda kukazuka vurugu nchini Zambia wakati huu nchi hiyo inapojiandaa kwa uchaguzi mwezi ujao.
Uvamizi huo wa polisi katika makaazi hayo unafanyika siku mbili tu baada ya marufuku ya kampeni kuondolewa katika baaadhi ya maeneo nchini humo.
Bw Mwamba,ambaye hakuweko nyumbani wakati wa uvamizi huo wa polisi anasema wajukuu wake ni miongoni mwa waliojeruhiwa na wamepelekwa hospitali.
Bw. Mwamba ni mgombea mwenza wa Bw. Hakainde Hichilema, anaegombea kiti cha urais kwa tiketi ya chama cha United Party for National Development (UPND) .
Rais wa sasa Edgar Lungu, wa chama cha Patriotic Front, anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa kambi ya Bw.Hichilema.
Post a Comment