0
Maafisa wa Korea Kusini wameushutumu utawala wa Korea Kaskazini wakisema umefufua vita baridi.
Wanatoa mfano wa hivi majuzi ambapo, kulikuwa na matangazo kutoka redio Pyongyang ya Korea Kazkazini.
Redio hiyo ilipeperusha msururu wa namba zisizoeleweka vyema ambazo Korea Kusini wanasema huenda ni mbinu ya kuwasiliana na majasusi wao ambao huenda wanajificha nchini Korea Kusini.
Msemaji wa wizara ya maswala ya utangamano huko Korea Kusini anasema hiyo ni mbinu mojawapo iliyokuwa ikitumika wakati wa enzi za vita baridi kuwasiliana na majasusi ambao huweza kubaini nambari hizo za siri, na kufahamu ujumbe unatolewa.
Tangazo mojawapo kama hilo lilifanywa usiku wa manane na sauti ya mtangazaji wa kike akitoa nambari hizi - "ukurasa 459 namba 35, ukurasa 913, namba 55, na kadhalika... tena hata akaendelea kutoa maelezo na kusema "Nawapa Kazi Namba 27, ma-ajenti wa utafiti."
Korea kusini imeitaka Korea Kazkazini kukomesha mara moja uchokozi huo.
Maafisa wa kijasusi wa Korea Kusini wanajikuna vichwa kujaribu kubaini maana ya ujumbe huo unaotolewa kwa vitendawili.
Lakini wachanganuzi wanashangaa ni kwa nini Korea Kazkazini watumie mbinu hiyo ya kizamani ilhali siku hizi ziko mbinu nyingi za kuwasilisha ujumbe kwa urahisi kupitia mitandao ya intaneti.
KimImage copyrightAP
Image captionRais wa Korea Kaskazini amekuwa akitoa vitisho kwa Korea Kusini na Marekani
Au ni mbinu nyengineyo ya kutoa vitisho tu kama vile Korea Kaskazini inavyofanya kupitia majaribio ya makombora ya kinyuklia.
Mwezi huu Korea Kusini na Marekani waliamua kupeleka mitambo ya hali ya juu ya kujilinda dhidi ya makombora katika maeneo hayo ya Korea jambo lililoudhi sana utawala wa Pyongyang.
Utawala wa Korea Kaskazini pia umewahi kueneza uvumi na propaganda ya kusema wanaweza kutumia ndege zisizoonekana kwenye mitambo ya rada kushambulia uwanja wa ndege wa Seoul.
Kama hilo linawezekana au la ni suala la mjadala lakini ni mambo kama hayo yanayouongezea wasiwasi utawala wa Korea Kusini .

Post a Comment

 
Top