1


TANZANIA itaanza kuuza masafa ya mawasiliano kwa njia ya mnada kuanzia mwakani.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema hayo jana baada ya kumaliza mkutano wake na Mtendaji Mkuu wa Nchi wanachama wa Mawasiliano katika Jumuiya ya Madola, Dk Shola Taylor.
“Kuanzia mwakani mnada wa masafa utaanza, zoezi hilo ni jipya hatuwezi kufanya makosa, nina imani tutapata fedha za kutosha, ” alisema.
Waziri Mbarawa alisema masafa hayo yalipatikana baada ya Tanzania kutoka analojia kwenda digitali ambapo masafa 700- 816 yako wazi.
Alisema baadhi ya nchi barani Afrika zimeanza kuuza masafa kwa njia ya mnada na sasa Tanzania itaanza mwakani na kuongeza kuwa nchi za Ghana na Nigeria zimefanikiwa katika hilo na Tanzania inataka kufanya kitu kutokana na mafanikio hayo.
Alisema watakaonunua masafa watatakiwa kuyatumia, vinginevyo wanaweza kunyang’anywa masafa hayo na kuwa wanataka kujipanga vizuri ili sekta hiyo ipate fedha na anaamini Tanzania itafanikiwa katika hilo.
Alisema pia Jumuiya hiyo imekuwa na mikakati mizuri ya ushirikiano kwenye masuala ya kukabiliana na uhalifu wa kimtandao na jinsi ya kushirikiana.
Alisema nchi nyingi zimeweka mikonga ya taifa na kama serikali watapeleka huduma kwenye hospitali na maeneo mbalimbali ya nchi, pamoja na kutengeneza maudhui, kwani katika nchi hakuna maudhui ya kutosha na kutakuwa na mkakati wa kutosha wa kuweza kutayarisha maudhui kwa njia ya kiswahili ili watu wengi wanaufaike na elimu inayotolewa.
Naye Dk Taylor aliipoongeza Tanzania kwa kupiga hatua katika sekta ya mawasiliano na kuongeza kuwa nchi za Afrika zimeanza kuuza masafa kwa njia ya mnada na katika hilo anaamini Tanzania itafanikiwa kutokana na kupiga hatua katika nyanja ya mawasiliano.

Post a Comment

 
Top