0
Mili miwili ya wanamuziki 10 waliokufa maji katika ziwa Victoria baada ya dau lao kuzama imepatikana.
kulingana na gazeti la The Standard,mili hiyo hatahivyo itasalia kuwepo katika ufukwe wa bahari hadi pale miili minane iliosalia ipatikane kulingana na tamaduni za eneo hilo.
Kuomboleza kumepigwa marufuku kwa muda kutokana na hofu kwamba huenda kukaleta bahati mbaya na kuathiri juhudu za kuitafuta miili hiyo.
Wingu la kusikitisha bado limetanda katika ufukwe huo huku miili ya wanachama hao wa bendi ya Boyieta Ohangla ambao maisha yao yalisitishwa mara moja na mawimbi makali katika ziwa Victoria ilipatikana huku operesheni ya kuisaka miili mingine ikiendelea.
Jamaa za wanachama hao walilazimika kuzuia machozi ili kuitizama miili ya wapendwa wao.
Kulingana na Odida Buoga mwenye umri wa miaka 70 ambaye ni mwenyekiti wa baraza la wazee wa Kiluo hakuna mtu anayepaswa kulia kabla ya miili hiyo haijapatikana.
''Ni utamaduni wetu kwamba mtu anapofariki jamii yake ni lazima ipige kambi katika ufuo wa ziwa hadi pale mwili unapopatikana'',mzee buoga aliliambia gazeti la The Standard nchini Kenya.
Image captionZiwa Victoria
Ameelezea kwamba watu hawafai kulia kwa hofu kwamba kilio hicho huenda kikazuia miili ama mwili huo kupatikana.
Anasema kwamba wakati msakaji wa mwili anapopata mwili huo ndani ya maji ama katika ufuo ,hulazimika kuufunga kamba mwili huo na kuuvuta hadi ufuoni na baadaye kuwajuza watu wa familia yake.
Kulingana na gazeti la The Standard,iwapo mtu atashindwa kufanya hivyo basi inasemekana kwamba huenda akaandamwa na mazingaombwe.
Mzee huyo anasema kuwa mtu yeyote atakayepata mwili atalazimika kuandamana na mwili huo hadi nyumbani kwa familia ya mfu huo ili achinjiwe kuku kwa lengo la kujitakasa.
''Kuku ama mbuzi unayepewa sio wa kufugwa bali ni kumchinja na baadaye umfanye kitoweo ili kujitakasa''.Anasema kuwa mmiliki wa boti iliyozama pia naye anapewa kuku ili kujitakasa.
Iwapo hilo halitofanyika basi boti hiyo huonekana kama yenye bahati mbaya na hivyobasi haiwezi kutumika tena.
Image captionUvuvi Ziwa Victoria
Kwa lengo la kuomboleza na familia ya marehemu wavuvi huwa hawaruhusiwi kufanya uvuvi,badala yake hutumia boti zao kuisaka miili.
Maafisa wa polisi pia walizuiliwa kuchukua miili hiyo hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti na badala yake wameagizwa kusubiri hadi miili yote itakapopatikana.

Post a Comment

 
Top