0


Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Massauni
MKOA wa Dar es Salaam na hasa manispaa za Kinondoni na Ilala zimetajwa kuwa vinara wa ajali za barabarani kati ya mwaka 2013 na 2015. Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni, alisema mikoa ya Kipolisi ya Kinondoni na Ilala imeongoza katika ajali hizo, huku Temeke ikiongoza kwa mwaka 2015.
Masauni alisema mwaka 2013 zilitokea ajali 23,842 zilizosababisha vifo 4,002 na majeruhi 20,689, mwaka 2014 ajali 14,630 zilizosababisha vifo 3,760 na majeruhi 14,530. Kwa mwaka 2015, ajali zilikuwa 8,337 zilizosababisha vifo 3,468 na majeruhi 9,383.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri, mikoa iliyoongoza kwa ajali mwaka 2013 ni Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni uliokuwa na ajali 6,589 na Mkoa wa Kipolisi wa Ilala uliokuwa na ajali 3,464. Alisema mikoa iliyokuwa na ajali chache ni Simiyu ajali 67 na Tanga ajali 96.
“Mwaka 2014, mikoa iliyoongoza kwa ajali ni Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni ajali 3,086 na Mkoa wa Kipolisi wa Ilala ajali 2,516 na mikoa iliyokuwa na ajali chache ni Kagera ajali 29 na Simiyu ajali 55,” alieleza Naibu Waziri.
Alisema kwa mwaka 2015, Mkoa wa Kipolisi wa Ilala ajali zilikuwa 1,431 na Temeke ajali 1,420 na mikoa iliyokuwa na ajali chache ni Rukwa ajali 53 na Arusha ajali 53. Naibu Waziri alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Biharamulo, Oscar Mukasa (CCM) aliyetaka kufahamu takwimu za ajali kuanzia mwaka 2013 hadi 2015 kitaifa na mikoa iliyoongoza na iliyokuwa na ajali chache kwa kipindi hicho.

Post a Comment

 
Top