Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya
Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mh. Dk.Hamisi Kigwangalla ameendelea na
ziara yake ya kikazi ya kukagua huduma za Afya ‘Imarisha Afya’ katika
Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali mbalimbali kwenye mikoa ya
Rukwa, Katavi pamoja na Tabora.
Akiwa katika mkoa wa Rukwa, Dk.
Kigwangalla aliweza kutembelea Hospitali ya Sumbawanga ambayp ni ya Mkoa
wa Rukwa na kujionea mambo mbalimbali huku akiwapongeza kwa namna
walivyoboresha huduma zao ikiwemo ile ya Maabara, Chumba cha upasuaji na
huduma zingine ambapo aliwaagiza kuhakikisha wanakuwa na hakiba ya
kutosha ya damu salama kwa ajili ya dharura kwa wagonjwa wa ukanda huo.
Mbali na Hospitali ya Mkoa wa Rukwa,
pia aliweza kutembelea kituo ca Laela ambapo pia mbali ya kujionea
utendaji kazi wa kituo hicho alipongeza juhudi za Mbunge wa jimbo la
Kwera, Mh. Ignas Alloyce Malocha kwa kushirikiana na wananchi wake
katika masuala ya huduma za Afya.
Ziara hiyo katika mkoa wa Rukwa,
aliweza kumalizia katika Kituo cha Afya Wampembe kilichopo Wilayani
Nkasi ambapo alijionea shughuli mbalimbali ikiwemo huduma za Upasuaji
hata hivyo aliutaka uongozi wa kituo hicho ambacho kipo mwambao wa Ziwa
Tanganyika kuhakikisha wanakamilisha mifum ya maji safi na salama ndani
ya kituo pamoja na kuboresha huduma za Maabara na usafi kwa ajumla.
Akiwa katika Mkoa wa Katavi, Dk.
Kigwangalla aliweza kufanya ziara ya kushtukiza kituo cha Afya
Inyonga,kilichopo Mlele majira ya Saa Sita mchana na kuweza kukagua
maeneo mbalimbali ikiwemo Chumba cha Maabara, Chumba cha Upasuaji na
wodi ya akina mama wanaosubiria kujifungua.
Hata hivyo, Dk. Kigwangalla amemtaka
Kaimu Mganga Mkuu wa Kituo hicho kumuandikia maelezo juu ya kutokuwepo
kwa watoa huduma kwenye jingo la chumba cha upasuaji na eneo la wodi ya
akina mama wanaosubiria kujifungua kwani licha ya kufika hapo hakukuta
mtoa huduma hata mmoja kwa wakati huo hali ambayo inaweza kuleta hatari.
“Nataka kupata maelezo kwa maandishi.
Kwa nini hakukua na watoa huduma ndani ya Chumba cha upasuaji na kule
kwa wodi ya wamama wajawazito. Nilifika kuwakagua kwa upande wa Maabara
nimekuta safi mumeweza kuboresha huduma na mumezingatia maelezo yangu
niliyoyatoa kipindi nilichofika kukagua mwaka jana. Lakini pia hali
niliyoikuta katika maeneo hayo niliyotembelea bila kuwakuta wahusika hii
ni hatari nitahitaji maelezo ya kimaandishi” alieleza Dk. Kigwangalla
wakati akitoa maagizo kwa Kaimu Mganga Mkuu wa kituo hicho.
Aidha, akiwa katika mkoa wa Tabora,
aliweza kutembelea eneo la jengo linalojengwa Hospitali ya Wilaya ya
Uyui na baadae aliweza kumalizia ziara yake katika Zahanati ya Isikizya
ambapo aliagiza Mkurugenzi wa Wilaya ya Uyui kuhakikisha wanatenga
bajeti pamoja na kushirikiana na nguvu za wananchi na mbunge wa jimbo
hilo wanajenga majengo ya kulazwa wagonjwa, chumba cha upasuaji, maabara
na miundombinu mingine ili Zahanati hiyo ije kupanda na kuwa Kituo cha
Afya kwani kinahudumia eneo kubwa katika mji huo wa Isikizya ambayo hipo
ndani ya Makao makuu ya Wilaya hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment