0
Rais wa Marekani Donald Trump amejaribu kujitetea na kufafanua ni kwa nini alirejelea kisa cha ukosefu wa usalama nchini Sweden alichosema kilitokea Ijumaa, ilhali hakukuwa na kisa kama hicho.
Akihutubia mkutano wa hadhara Jumamosi, alisema, "tazama yaliyotokea Sweden usiku wa kuamkia leo", alipokuwa anataja maeneo ya Ulaya ambayo yamekumbwa na mashambulio ya kigaidi.
Hakuna tukio lolote lililoripotiwa nchini Sweden wakati huo.
Taifa hilo limeitaka serikali ya Marekani kutoa ufafanuzi.
Bw Trump aliandika kwenye Twitter baadaye Jumapili kwamba alikuwa akirejelea taarifa kwenye runinga.
Alisema taarifa hiyo ilipeperushwa na kituo cha habari cha Fox News lakini hakusema ni lini.
Huenda alikuwa anarejelea makala iliyopeperushwa na Fox News Ijumaa usiku, ambayo iliangazia tatizo la wahamiaji na uhalifu nchini Sweden.
Licha ya kusema kisa "kilitokea usiku wa kuamkia jana Sweden", msemaji wa White House Sarah Huckabee Sanders alisema kwamba Bw Trump alikuwa anazungumzia ongezeko la visa vya uhalifu kwa jumla na wala si kisa fulani.
Waziri mkuu wa zamani wa Sweden Carl Bildt alikuwa miongoni mwa waliomkejeli Bw Trump na kupendekeza kwamba huenda "amekuwa akivuta" kitu.
Former Swedish Prime Minister Carl Bildt tweet reads:
Watu katika mitandao ya kijamii walimkejeli kiongozi huyo wa Marekani, wakiandika visa vya kufikiria tu vilivyohusisha asasi za Sweden, miongoni mwa hizo kundi la muziki la Abba na maduka ya samani Ikea.
'Taarifa iliyopeperushwa'
Jumapili, Bw Trump kupitia Twitter alisema: "Tamko langu kuhusu yanayotendeka Sweden lilitokana na taarifa iliyopeperushwa katika @FoxNews kuhusu wahamiaji & Sweden."
Taarifa hiyo ya Fox News iliangazia visa vya uhalifu wa kutumia bunduki na ubakaji ambavyo vimetokea tangu Sweden ilipoanza kuwapokea kwa wingi wahamiaji waliokuwa wanatafuta hifadhi mwaka 2013.
Fox News ni miongoni mwa vituo anavyovipenda zaidi Donald Trump.
Rais Trump alizungumzia Sweden wakati wa mkutano mkubwa wa hadhara Florida ambapo alivishambulia tena vyombo vya habari na kudai vinaeneza taarifa za uongo.
"Tazama yanayotokea Ujerumani, tazama yaliyotokea usiku wa kuamkia leo Sweden," alisema.
"Sweden, nani anaweza kuamini hili? Sweden. Waliwapokea wahamiaji kwa wingi. Sasa wanapata matatizo mengi kulivyo walivyofikiria. Tazama yanayotokea Brussels, tazama yanayotokea maeneo mengine duniani. Tazama Nice, tazama Paris."

Nini kilitokea Sweden Ijumaa?

Ukweli ni kwamba hakuna kisa cha ugaidi kilichoripotiwa Ijumaa.
Tovuti ya Aftonbladet ya Sweden ilitoa muhtasari wa yaliyotokea siku hiyo ambapo ni:
  • Mwanamume alijiteketeza mjini Stockholm
  • Mwanamuziki mashuhuri Owe Thornqvist akatatizwa na hitilafu za kimitambu akijiandaa kwa tamasha
  • Mwanamume akafariki katika ajali kazini
  • Barabara zikafungwa kaskazini mwa Sweden kutokana na "hali mbaya ya hewa"
  • Polisi wakaonekana wakikimbiza gari moja katikati mwa Sweden ambalo inadaiwa lilikuwa linaendeshwa na dereva mlevi
Katika mtandao wa Twitter, watu walitumia kitambulisha mada #lastnightinSweden (usiku wa kuamkia leo Suweden) ambacho kilivuma sana Twitter.
Tamko la Donald Trump lilitokea wiki chache baada ya mmoja wa washauri wake wakuu, Kellyanne Conway, kurejelea mauaji ambayo hayakutokea ambayo aliyaita mauaji ya Bowling Green.
Sweden, ina watu 9.5m, na imewapokea wakimbizi na wahamiaji 200,000 katika miaka ya karibuni, zaidi zaidi ukilinganisha na idadi ya raia wake kuliko nchi nyingine zote za Ulaya.
Hakuna kisa chochote cha ugaidi kimeripotiwa tangu Sweden ifungue mipaka yake 

Post a Comment

 
Top