0
Benchi la ufundi la Simba limeishitukia kasi ya Yanga na haraka kocha msaidizi wa timu hiyo, Jackson Mayanja amesema wanatakiwa kufunga mabao mengi zaidi katika mechi zao za Ligi Kuu Bara.
Lakini mwanzo alianza kocha mkuu, Joseph Omog na msaieizi wake Mayanja raia wa Uganda ameitoa kauli hiyo wakati leo timu yake inacheza mechi ya ligi kuu dhidi ya Mwadui FC kwenye Uwanja wa Kambarage huko mkoani Shinyanga.

Simba wameshitushwa na kasi ya Yanga baada ya kupata mabao 10 katika mechi mbili dhidi ya Kagera Sugar waliyoshinda mabao 6-2 na ile dhidi ya JKT Ruvu waliyoshinda mabao 4-0.

Mayanja alisema wanataka kufunga mabao mengi ambayo mwishoni mwa ligi kuu yanaweza kuwasaidia kutokana na ushindani uliopo kwenye ligi hiyo.
Mayanja alisema, kikubwa hawataki kuona wapinzani wao Yanga wakiwakaribia au kuwafikia kwenye msimamo wa ligi, hivyo ni lazima watoke na pointi sita Shinyanga dhidi ya Mwadui na Stand United.

“Tumeshitushwa na kasi ya wapinzani wetu Yanga ya kupata ushindi wa mabao kumi kwenye mechi mbili walizozipata hivi karibuni.

“Hivyo, kikubwa tunachotakiwa kukifanya sasa ni kushinda kila mechi tutakazozicheza tena ushindi wa mabao mengi ili mwishoni mwa ligi yatutasaidie pale tutakapokuwa na pointi sawa na timu nyingine.  

“Washambuliaji wetu wanatakiwa kuongeza umakini ndani ya uwanja kwa kutumia vizuri kila nafasi tutakayoipata kwa kufunga mabao mengi,” alisema Mayanja.

Naye mshambuliaji mkongwe wa Mwadui, Jerry Tegete alisema: “Maandalizi ya timu yetu yanaenda vizuri na kwenye mechi hii tunahitaji pointi tatu ili tujiweke kwenye nafasi nzuri katika msimamo.”

Post a Comment

 
Top